Kampuni ya Raha, imetozwa faini ya Sh. bilioni 11 kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo kutumia masafa ya mawasiliano ya redio bila leseni halali ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), tangu Machi 24 mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, ametangaza adhabu hiyo jana Agosti 28,2020 jijini Dar es Salaam, mbele ya waandishi wa habari, baada ya kuthibitisha makosa yaliyofanywa na Kampuni ya Raha.
Amesema kati ya fedha hizo, waliitoza kampuni hiyo faini ya Sh. bilioni 11.850 kwa kutumia masafa ya mawasiliano ya redio katika wigo wa 1452-1482 MHZ.
Amesema pia Sh. milioni 10 kwa kujenga miundombinu ya mfumo wa mawasiliano, kuendesha na kutoa huduma za mawasiliano katika mkoa wa Mtwara bila leseni kutoka TCRA.
Kilaba amesema kampuni hiyo pia ilitozwa faini ya Sh. milioni 5 kwa kushindwa kujenga, kusimika, kuendeleza, kuendesha na kuwezesha upatikanaji wa miundombinu ya mawasiliano mkoa wa Tanga kwa mujibu wa leseni yake.
Kadhalika kampuni hiyo imetozwa faini ya Sh. milioni 5 kwa kushindwa kuwasilisha kwa TCRA taarifa za ukaguzi wa mahesabu yake ndani ya miezi sita na Sh. milioni 5 nyingine kwa kushindwa kuwasilisha mpango mkakati wa mwaka wa kuendeleza rasilimali watu.
Kilaba amesema faini ya Sh. milioni 10 ilitozwa pia kwa kushindwa kutimiza masharti ya leseni, kushindwa kuomba upya leseni kwa muda uliopangwa.
“Raha Limited ilishindwa kutimiza masharti yote yaliyotolewa ndani ya siku 90 TCRA itachukua hatua zaidi za kiudhibiti dhidi yake,” amesema Kilaba.
Kilaba amefafanua kuwa, TCRA ilifikia maamuzi hayo chini ya kifungu 48 (2) cha Sheria yake sura ya 172, iliyofanyiwa mapitio ya mwaka 2017, baada ya kuzingatia utetezi uliotolewa mbele yake na Kampuni ya Raha.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment