Mabalozi: Tanzania, Afrika Imepoteza Msuluhishi Nguli Wa Amani

 Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wameendelea kujitokeza kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa na kumuelezea kuwa ni kiongozi mahiri na msuluhishi nguli wa amani barani Afrika na duniani.

Mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, baadhi ya mabalozi hao wakaelezea walivyoguswa na msiba wa Mkapa na kusema Tanzania imepoteza kiongozi na msuluhishi nguli wa amani barani Afrika na duniani.
 
Kwa upande wake, Balozi wa Zambia nchini Mhe. Benson Keith Chali amesema kuwa Zambia wameguswa sana na msiba kwani Tanzania na Zambia ni ndugu, “toka mwanzoni Nyerere na Kaunda walikuwa ndugu na sisi tumeendelea kuwa ndugu na unapopoteza ndugu unaumia sana. Sisi kama Zambia kwa kweli tumepokea kwa masikitiko makubwa tarifa za kifo cha Mzee Mkapa,” .

“Tutamkumbuka Mzee Mkapa kama kiongozi aliyesimamia amani maeneo mbalimbali barani Afrika ikiwemo Kenya, Burundi, Congo DRC, na kwingineko duniani,” amesema Mhe. Keith Chali   
 
Mhe. Keith Chali ameendelea kusema kuwa “Sisi kama Zambia tunatoa sana pole kwa familia yake, Serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla ……tunaomboleza wote msiba huu mzito,”.

Nae Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Dissing-Spandet amesema kuwa Rais Mstaafu Mzee Mkapa alikuwa kiongozi mahiri kwa Tanzania lakini pia alikuwa rafiki na mfano wa kuigwa na mataifa mbalimbali.
 
“kwetu sisi kama Denmark alikuwa rafiki na tutaendelea kumkumbuka daima kwa upendo wake,” Amesema Mhe. Mette.

Aidha, nae Balozi wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal amesema kuwa Mzee Mkapa alikuwa mtetezi wa amani barani Afrika na atakumbukwa kwa mema aliyoyafanya kwani aliyafanya kwa jitihada na weledi wa hali ya juu, Mungu ampumzise kwa Amani.
 


from MPEKUZI

Comments