Freeman Mbowe atuma salamu za rambirambi Kifo Cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais mstaafu Benjamin William

 Mbowe ametuma salamu hizo kwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mama Anna Mkapa, familia na Watanzania kutokana na kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo Ijumaa tarehe 24 Julai 2020.

-==>Salamu  za Mbowe alizozitoa ni hizi hapa;

Sina maneno ya kutosha kuelezea kushtushwa kwangu, na nina hakika kwa Watanzania wengi kwa kupata taarifa za Mzee wetu, Kiongozi wetu na alama mojawapo muhimu kwa Taifa letu, Mzee Benjamin William Mkapa kutangulia mbele ya haki.

Familia nzima ya Chadema na Familia yangu binafsi, tunaungana nawe, Mheshimiwa Rais na Familia nzima ya Hayati Mzee Benjamin William Mkapa, katika kuomboleza msiba huu mkubwa huku tukimshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha aliyomkirimu mja wake huyu kwa miaka yote na zaidi kwa utumishi wake kwa Taifa la Tanzania na Jamii ya Kimataifa.

Kupitia maisha yake, Hayati Rais Mstaafu Mhe. Mkapa ameacha alama ya uongozi kwa taifa letu kupitia nafasi mbalimbali za utumishi wa umma alizoshika wakati wa maisha yake kuanzia wakati wa Serikali ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Alikuwa kielelezo maridhawa cha nguvu ya kidiplomasia katika kujenga mahusiano ya Kimataifa na hakika si Tanzania pekee, bali jamii nzima ya Kimataifa imempoteza Mwanadiplomasia mahiri na msuluhishi wa Kimataifa.

Namtambua Mzee Mkapa kama mtu aliyekipenda sana Chama chake cha CCM, na aliyekuwa tayari kukilinda kwa nguvu za ziada hata pale alipotegemewa kwenda hatua moja zaidi kuonyesha kwa vitendo dhana na thamani ya Demokrasia ya kweli kwa Taifa letu, kipekee akiwa Rais aliyeko madarakani au hata baadaye kama Rais Mstaafu.

Kama mwandishi mbobezi, kupitia kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’, Hayati Mhe. Mkapa ameacha alama kubwa kwa kizazi cha sasa na vingi vijavyo na kutoa funzo kwa viongozi wengine kuelewa kuwa uongozi ni dhamana ambayo wanapaswa kuitumikia kwa unyeyekevu na tahadhari kubwa wakiwa madarakani kwa manufaa ya wananchi na kuepuka kujutia baada ya kuachia nafasi hizo.

Kwa mara nyingine tena na kwa niaba ya viongozi na wanachama wenzagu na wapenzi na wafuasi wa Chadema na mamilioni ya Watanzania tunaowaongoza, natuma salaam za rambirambi na kutoa pole kwa familia yake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Rais wa Zanzibar na serikali zote mbili na chama chake kwa msiba huu mzito kwa taifa letu.

Mwenyezi Mungu afanyike faraja wakati wote wa maombolezo na majonzi ya msiba huu, na zaidi akaipumzishe pema peponi roho ya Mzee wetu mahali pema peponi.

Aidha, kwa kipekee na umuhimu mkubwa, tunamwombea uvumilivu na subira Mama yetu Anna Mkapa na familia yote katika kukabiliana na pengo kubwa aliloacha Mzee wetu!

Familia ya Chadema inaungana kwa kila hatua na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huu huku tukikumbushana kwa unyenyekevu mkubwa kuwa maisha yetu, umoja wetu na upendo miongoni mwetu yapaswa kuwa msingi wa utaifa wetu na kamwe si vyama vya siasa.

Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa, jina lake lihidimiwe!

Pumzika kwa amani Mzee Mkapa!


from MPEKUZI

Comments