Wigo Mpana Sekta Ya Kilimo Kwenye Utunzaji Mazingira Na Uendelezaji Viwanda Utumike Kupunguza Utegemezi Wa Ajira Serikalini

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya  amesema wigo mpana ulipo katika sekta ya Kilimo kwenye utunzaji wa mazingira na uendelezaji wa viwanda utumike kupunguza utegemezi wa Ajira serikalini kwa wahitimu wa vyuo vya Kilimo.

Akiongea leo Mara alipotembelea chuo Cha Taifa Cha sukari NSI kilichopo Kidatu Kilombero mkoa wa Morogoro Bw.Kusaya amesema vyuo hivyo vitumie taaluma walizonazo ikiwemo uzalishaji wa mkaa mbadala na karakana zilizopo kwenye vyuo vyote vya Kilimo kuongeza taaluma na kuweza kujiajiri pindi wanapohitimu vyuo  hivyo.

Amesema kwa kuwa Kilimo hakiwezi kutenganishwa na utunzaji wa mazingira na uendelezaji wa viwanda vidogo  ni lazima wanafunzi wanapohitimu katika vyuo vya Kilimo wawe ni Chachu katika kuendeleza viwanda vidogo na utunzaji wa mazingira.

Aidha akiongea na mwanafunzi anayejishughulisha na utengenezaji wa mkaa mbadala  Katibu Mkuu ameahidi kumkutanisha Bi Upendo Emanuel mwanafunzi wa stashahada katika chuo hicho na wadau mbalimbali wanajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa hiyo ili kuongeza ujuzi.

“Nataka wanafunzi kutoka vyuo vya Kilimo wawe na wigo mpana wa kujiajiri kwa kuhakikisha karakana za utengenezaji wa vipuri mbalimbali ambazo zipo katika vyuo vyetu na taaluma za utunzaji wa mazingira kwa kutengeneza mkaa mbadala iwe ni Chachu kwa wahitimu kuweza kujiajiri.”Alisema Bw.Kusaya.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema  chuo kishirikiane na viwanda vya sukari na wadau wengine katika kutatua tatizo la upungufu wa sukari nchini ambalo limekuwa likijitokeza Mara kwa mara hapa nchini.

“Tuandae mkutano utakaojumuisha chuo Cha Taifa Cha Sukari wadau wa uzalishaji wa sukari na wataalamu wengine ili kuhakikisha tatizo hili  linakwisha” alisema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu amemtaka Mkuu wa chuo hicho  Eng.Julius Deteba kuandaa andiko litakalo onesha mahitaji muhimu  ili Wizara iweze kusaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu na majengo ya chuo hicho.

Aidha Katibu Mkuu ameshauri Chuo hicho kushirikiana na wadau ili kupata eneo litakalo tumika kuanzisha shamba darasa la Kilimo Cha miwa.

Akihitimisha kikao chake na watumishi wa chuo hicho amevitaka vyuo vya  Kilimo kujiendesha kibiashara ili kuweza kutatua changamoto zinazozikumba Taasisi hizo.


from MPEKUZI

Comments