Waziri wa Fedha Dkt. Mpango Aagiza Matumizi Ya Fedha Ujenzi Kituo Cha Afya Munzeze Kigoma Yachunguzwe

Na. Josephine Majula na Peter Haule, WFM, Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameagiza kufanyika uchunguzi wa kina wa matumizi ya zaidi ya shilingi milioni 400 zilizotumika kujenga Kituo cha Afya  Munzeze, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, baada ya kutoridhishwa na ubora wa majengo ya Kituo hicho.

Dkt. Mpango alitoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya ambacho kikikamilika kinatarajiwa kutoa huduma kwa zaidi ya wakazi 25,000 wa Kata hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayopatiwa fedha na Serikali.

 “Nakuagiza Mkuu wa Wilaya  ya Buhingwe uanze kufuatilia matumizi ya fedha hizo na nitatuma  timu ya uhakiki ili tuhakikishe kwamba shilingi milioni 400 zilizotolewa na Serikali zilitumika vizuri au la”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa uhakiki huo ukibaini ubadhirifu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watu wote waliohusika na ubadhirifu huo na kuonya kuwa huu si wakati wa  kubembelezana.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina alisema atayafanyia kazi maelekezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, kwa kuwa tayari alifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa Ujenzi wa Kituo hicho.

Aidha alimshukuru Dkt. Mpango kwa kufanya ziara katika Wilaya hiyo katika jitihada za kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kikamilifu katika miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Munzeze ameiomba Serikali itoe kiasi kingine cha shilingi milioni 123 kwa ajili ya kununua vifaa tiba ili Kituo hicho kianze rasmi kutoa huduma kwa wananchi mapema mwezi Julai, 2020.

Bw. Conrad alisema ujenzi wa Kituo hicho ulitakiwa kukamilika  Machi, 2019 lakini ilishindikana kutokana na uwepo wa mvua nyingi uliosababishja kushindwa kusafirisha vifaa kwenda eneo la ujenzi na changamoto ya ununuzi.

Kituo hicho cha Afya Munzeze kikikamilika kitaongeza idadi ya watu wanaohudumiwa katika zahanati iliyopo hivi sasa wapatao 16,000 hadi kufikia takribani wakazi 25,000 kutoka vijiji vine vinavyounda kata hiyo vya Munzeze, Kishanga, Kigogwe na Murungu.

Katika hatua nyingine Dkt. Mpango amewaahidi wananchi wa mkoa wa Kigoma kwamba Serikali itajenga barabara inayoanzia katika Mpaka wa Burundi na Tanzania kupita katika maeneo ya Wilaya ya Buhigwe, Kasulu, Kibondo na Kakonko, hivyo kuwawezesha wakazi hao kusafirisha bidhaa katika nchi jirani ikiwemo Uganda na Burundi.

“Baada ya muda mfupi barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha Lami kwani tayari Serikali imeingia mkataba na wakandarasi wane baada ya kupata fedha kutoka mfuko wa b Abudhabi na Kuwait”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma watakuwa na uwezo wa kufanya biashara ya mazao likiwemo zao la Tangawizi katika mikoa jirani na pamoja nan chi za Burundi na Uganda.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments