Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kutumia ramani zilizoandaliwa na kutolewa na Wizara ya Ardhi kupitia idara yake ya Upimaji na Ramani kwa kuwa ndiyo yenye jukumu la kutafsiri mipaka ya nchi.
Akizungumza wakati akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus Mwengela ramani mbili za Tanzania pamoja na ile ya mkoa wa Songwe jana, Dkt Mabula alisema, Wizara kupitia idara yake ya upimaji na ramani ndiyo yenye mamlaka ya kuandaa na kutoa ramani nchini tofauti na zile zinazotolewa na watu wengine ambazo wakati mwingine zinakuwa na upotoshaji wa mipaka.
Alisema, katika kuepukana na sintofahamu inayoweza kutokea, halmashauri nchini zinapaswa kutumia ramani zinazotolewa na wizara ya ardhi na kuzisambaza katika shule za msingi na sekondari ili kuepuka aina yoyote ya upotoshaji unaoweza kutokea kwa wanafunzi.
‘’Ninaziomba halmashauri nchini kutumia ramani zinazotolewa na wizara kupitia idara ya upimaji kwa kuwa inatoa ramani zenye uhakika wa mipaka iliyotafsiriwa na wataalam tofauti na watu wengine wanaotoa ramani zenye upotoshaji wa mipaka ‘’ alisema Mabula
Naibu Waziri Mabula ambaye alizindua pia ofisi ya ardhi mkoa wa Songwe alisema, wizara yake itatoa ramani ya Tanzania kwenye mikoa yote na kubainisha kuwa ramani hizo ndizo zinazotakiwa kutumika kwa kuwa zina vielelezo vinavyokubalika.
Akigeukia uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa, Dkt Mabula alisema uzinduzi wa ofisi hizo ikiwemo ya mkoa wa Songwe ni jitihada za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi.
Kupitia uzinduzi wa ofisi hizo za ardhi aliwataka wananchi pamoja na wadau kuzitumia ofisi za ardhi za mikoa kupata huduma za sekta hiyo na kusisitiza kuwa wakifanya hivyo watakuwa wamekidhi matarajio ya Raisi Magufuli kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alionesha umuhimu na faida ya kuwa na hati ya ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Songwe na kuwaeleza kuwa wanaweza kuitumia katika shughuli za kiuchumi kwa kuchukulia mkopo benki na kutolea mfano wa jinsi hati ya kwanza kutolewa mkoa huo mwaka 1939 ambayo sasa iiko katika mkoa wa Songwe ilivyotumika kuchukulia mkopo na wamiliki wake.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus Mwengela alisema uanzishwaji ofisi za ardhi za mikao utausaidia mkoa wake kutatua migogoro ya ardhi kwa kuwa wananchi wake hawatahitaji tena kwenda umbali mrefu kama ilivyokuwa hapo nyuma.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi katika ofisi ya Ardhi mkoa wa Songwe Suma Mwakasitu alisema, ofisi yake ambayo tayari inazo hati na nyaraka mbalimbali zilizohamishiwa kutoka iliyokuwa ofisi ya kanda mkoa wa Mbeya itaendelea kufanya ziara kwenye wilaya nne inazohudumia kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusuiana na huduma inazotoa ili waweze kuitumia ofisi hiyo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment