Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida inatarajia kuwafikisha kwenye Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, Bahati Ilikunda Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kilimatinde na Mzazi mwenzake Haji Bwegege ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya Mwaka 2007.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye ofisi za PCCB, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema walipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja ambaye jina lake wamelihifadhi, kuwa Bahati Ilikunda wa Mahakama ya Mwanzo Kilimatinde Wilayani Manyoni anaomba Rushwa ya shilingi 350,000/=, ili atoe upendeleo kwa mtoa taarifa kwenye shauri la madai namba 03/2020, shauri ambalo lipo mbele yake .
Alisema Juni 28/ 2020 huko wilayani Manyoni maeneo ya kituo cha mabasi yaendayo Dodoma, Maofisa wa TAKUKURU walimkamata Haji Bwegege ambaye ni mzazi mwenzake na Bahati baada ya kupokea rushwa ya shilingi 170,000/= ikiwa ni sehemu ya shilingi 350,000/=zilizoombwa.
Alisema uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Singida umejiridhisha kuwa Haji Bwegege na Bahati Ilikunda wana mahusiano ya kifamilia (Wana mtoto waliyezaa pamoja) jambo linaloashiria uwezekano wa Bahati kumtumia Haji katika kupokea rushwa anazoziomba.
Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa shukrani za dhati kwa Idara ya Mahakama mkoani hapa kwa jinsi wanavyoshirikiana kwenye mapambano dhidi ya Rushwa kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Mkoa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment