Ole Nasha Avitaka Vyuo Kutoa Maelekezo Ya Kujikinga Na Corona Kwa Wanafunzi Bila Kuwatia Hofu

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amevitaka Vyuo vya Elimu ya Juu na vya Kati nchini vinavyoanza masomo Juni 1, 2020 kutoa maelekezo kwa wanafunzi ya jinsi ya Kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya CORONA bila kuwatia hofu.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kukagua namna Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilivyoandaa mazingira kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya CORONA kwa wanafunzi kuelekea kuanza masomo Juni 1, 2020.

Ole Nasha amesema virusi vya CORONA pamoja na kuwa vimepungua ni vizuri wanafunzi wakachukua tahadhari ya kuendelea kujikinga kwa kuwa haujaisha kabisa ikiwa ni pamoja na vyuo kufuata mwongozo wa serikali juu ya kuwakinga na kutoa elimu ya kujikinga kwa wanafunzi mara kwa mara ili kuhakikisha wanakuwa na afya njema wanapoendelea na masomo yao.

” Napenda kuvisisitiza Vyuo vyote vya Elimu ya Juu na Kati kuendelea kuwalinda wanafunzi kwa kufuata mwongozo uliotolewa na serikali pamoja na kuwapa wanafunzi elimu ya kujikinga bila ya kuwapa hofu,” amesisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri Ole Nasha ametumia fursa hiyo kuwatakia kila lakheri katika masomo wanafunzi wote wanaorudi Vyuoni na Shule na kuwataka kuwa na amani kwani Vyuo na Shule vimejipanga vema huku akiwataka wanafunzi hao kuzingatia miongozi ya kujikinga na kuwakinga wengine na maambukizi ya Virusi vya CORONA

Aidha, Naibu Waziri Ole Nasha amevitaka Vyuo vyote vya Elimu ya Juu na Kati kuandaa crash programu ya kutoa mafunzo kwa ajili ya kufidia muda wa masomo ili kuwawezesha kumaliza programu zilizopangwa kufanyika mwaka huu wa masomo

Amesisitiza kuwa crash programu hizo zinapaswa kuwa na ubora unaotakiwa na wala si kupunguza baadhi ya vitu ili kuwezesha kumaliza masomo na kufikia malengo ya mwaka yaliyowekwa.

“Naendelea kusisitiza kuwa crash programu zote zinapaswa kuwa na mafunzo yenye ubora uleule bila kupunguza mpango wowote. Vyuo vyote vinapaswa kufahamu kuwa hakutakuwa na mpango wowote wa kuendelea na programu za masomo ambazo hazijakamilika kwa katika mwaka huu wa masomo katika mwaka ujao wa masomo,”alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Profesa William Anangisye amesema Chuo Kikuu cha Dar ws Salaam kimejiandaa vyema katika kuhakikisha kinafuata mwongozo uliotolewa na serikali pamoja na kutoa elimu kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanakuwa salama katika mazingira ya chuo.

Profesa Anangise amesema sehemu zote za vyumba vya mihadhara, madarasa na mabweni kuna vifaa vya kutosha vya kunawa mikono ikiwa ni pamoja na kuyagawa madarasa yenye wanafunzi wengi.

Naye Mkuu wa Chuo Taaluma Bonaventure Rutinwa ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya Elimu ya Juu mapema kabla ya wanafunzi kuripoti chuoni .


from MPEKUZI

Comments