Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Chasema Corona Imepungua Sana Nchini, Champongeza Rais Magufuli

Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema kinafanya uchambuzi ili kubaini tiba mbadala ambazo zimetumika kwenye kukabiliana na virusi vya corona zina mchango gani katika kupungua kwa maradhi hayo Tanzania.

Rais wa chama hicho, Dk. Elisha Osati, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati MAT ikitoa tathmini ya kitaaluma kuhusu mwenendo wa corona.

Dk. Osati alisema tathmini waliyoifanya kuhusu mwenendo wa corona, wamebaini idadi ya wagonjwa imepungua kwa kiasi kikubwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma wakiwamo wanaohitaji kuwekewa oksijeni.

“Tunafanya uchambuzi ambao tutautoa unaolenga kujua kitu gani kimechangia na kwa namna gani kimepunguza corona Tanzania.

“Hatuwezi kudharau njia mbadala kwa sababu Watanzania wengi wanatumia miti shamba, wengi walikuwa wanatumia limao, tangawizi ambavyo vina vitamin C kwa wingi inayosaidia kujenga kinga ya mwili ili kupambana na wadudu mbalimbali wakiwamo corona.”

Alisema inawezekana tiba mbadala imekuwa na nafasi yake, hivyo uchambuzi kuhusu hilo utakuja.

“Watanzania tumewaelekeza vitu vingi vya kufanya watu wananawa mikono, wiki tatu mfululizo watu wamevaa barakoa, tunaamini hiyo imesaidia kupunguza tatizo pia. Kila kimoja tutakifanyia uchambuzi ikiwa ni pamoja matumizi ya tangawizi na limao,” alisema.

Akizungumza ugonjwa huo, Dk. Osati alisema Aprili sampuli zilizokuwa zikipelekwa maabara takribani 90 zilikuwa na corona wakati kwa sasa ni chini ya asilimia 10.

“Idadi ndani ya jamii zimepungua, kwa kuangalia idadi ya simu zinazopigwa kwa kuuliza au kuomba msaada wa kitaalamu kuhusu wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huu. Pia idadi ya vifo imepungua,” alisema.

Alisema MAT kimempongeza Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa kuwaongoza Watanzania katika kipindi hicho kigumu.

“Tunawapongeza madaktari na watumishi wa sekta ya afya kwa kuwa askari wa mbele kupambana na corona.

“Tunawaomba wagonjwa walioko nyumbani kwa matatizo ya corona au magonjwa mengine waje hospitali tuwahudumie, kwani corona imepungua kwa kiasi kikubwa. Madaktari tupo tayari kuwahudumia.”

Chama hicho kimewaeleza Watanzania kuwa ugonjwa huo bado upo, hivyo waendelee kuchukua tahadhari hasa wakati huu wa wanafunzi wanaporudi vyuoni.


from MPEKUZI

Comments