Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa ametoa rai kwa Taasisi ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo Tanzania (TEMDO) kuhakikisha wanawasaidia wajasiliamali wadogo na wa kati kubuni mashine za kutengeneza sukari pamoja na kuchakata katani ili kufungua fursa ya ajira na ongezeko la viwanda nchini.
Mhe. Bashungwa aliyasema hayo mkoani Arusha alipokuwa akizindua mashine 14 za kisasa zinazoendeshwa kwa mfumo wa kompyuta yaani CNC zikiwa na thamani ya shilingi milioni 600 zilizotolewa kwa fedha za Maendeleo za Serikali na za ufadhili wa shirika la kimataifa la UNIDO.
Akizungumza na watumishi wa taasisi hiyo Mhe. Bashungwa aliwataka TEMDO kuongeza kasi ya kubuni mtambo mdogo wa kuchakata miwa ili kupata sukari ili kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa wa bidhaa hiyo sokoni.
Aliongeza kwa kusema wafanyabiashara wanapandisha bei ya bidhaa hususani sukari sokoni, lakini endapo TEMDO itatengezeza mashine za kutengeneza sukari kwa wajasiriamali wadogo itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kusaidia upatikanaji wa sukari nchini.
Aidha amewataka pia kuongeza kasi ya kubuni mashine ndogo ndogo za kuchakata zao la mkonge kwa kiwango cha upatikanaji wa nyuzi ili kuwasaidia wajasiliamli wadogo kutengeneza nyuzi wao wenyewe ili waweze kuziuza na kujiongezea kipato badala ya hali ilivyo hivi sasa ambapo wakulima wanategemea wazalishaji wakubwa kununua bidhaa hiyo kwa kiasi kikubwa ambapo mkulima amekuwa hanufaiki.
Sambamba na hilo Mhe. Bashungwa alikabidhi barakoa zenye thamani ya Tsh.500,000 zilizotolewa na TEMDO kwa mkoa wa Arusha ikiwa ni sehemu ya kuungana na Serikali kupambana na ugonjwa wa Korona kwa watoa huduma ya afya.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, Prof. Fredrick Kahimba aliishukuru serikali kwa kuwawezesha kupata mashine hizo ambazo zitawezesha kuunda mitambo na mashine mbalimbali kwa urahisi zaidi kuliko awali.
Aliongeza kuwa “taasisi ya TEMDO imeendeleza shughuli mbalimbali zinazochangia maendeleo ya Viwanda Tanzania na kuwawezesha wakulima na wajasiliamali wadogo, wa kati na wakubwa kujipatia teknologia ya kuogeza uzalishaji mali.
Pia alimuomba Waziri Bashungwa kusaidia kuharakishwa uundwaji wa bodi mpya ya Wakurugenzi ya taasisi kwa kuwa liyokuwepo imemaliza muda wake.
Kwa upande wake bi Restuta Mrosso ambaye ni mnufaika wa utaalamu unaotolewa na TEMDO aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwapatia ujuzi wajasiriamali kutengeneza bidhaa mbalimbali na kuwasaidia kupata nembo ya Ubora (TBS).
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment