Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inatarajia kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake saba wakipinga hukumu na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 10 mwaka huu.
Kesi hiyo ilitajwa jana na kupangwa kutajwa tena mbele ya Lameck Mlacha Aprili 28 mwaka huu na rufaa itasikilizwa Mei 13 mwaka huu mbele ya Jaji Ilvin Mugetta.
Machi 10 Mbowe na wenzake nane walihukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 350 au kutumikia kifungo cha miezi mitano gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliokuwa yakiwakabili.
Uamuzi wa kuwatia hatiani ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi.
Mbali na Mbowe, viongozi wengine wa Chadema waliohukumiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko.
Wengine ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na aliewahi kuwa Katibu wa chama hicho Dk Vincent Mashinji, ambaye sasa amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo viongozi wote kwa nyakati tofauti walifanikiwa kulipa faini na kukwepa kutumikia kifungo hicho.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment