BMT kuandaa muongozo kuhusu ukomo wa wachezaji wa Nje nchini.

Na Shamimu Nyaki, WHUSM-Dodoma
Serikali haijatoa ukomo wa wachezaji kutoka nje kushiriki michezo hapa nchini bali imeibua mjadala kwa wadau ili watoe maoni yao.
 
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa ni hatua ya kuboresha na kuimarisha sekta ya michezo nchini. 
 
Ili kutekeleza mjadala huo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limepewa jukumu la kuendelea kuandaaa mwongozo utakaotumika kukusanya maoni kutoka kwa wadau kuhusu ukomo wa wanamichezo wa nje hapa nchini.
 
“Katika Hotuba ya Bajeti iliyosomwa hivi karibuni Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, hakuongolea idadi ya wachezaji kutoka nje wanaotakiwa kucheza nchini, bali aliagiza BMT kuandaa mjadala mpana katika kukusanya maoni kwa wadau wa michezo kuhusu namna bora ya kusajili wachezaji wa kigeni katika michezo yote hapa nchini” alisema Bw. Singo.
 
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo ambainisha kuwa Mhe.Waziri Dkt. Mwakyembe alisisitiza kuwa wanamichezo wote kutoka nje ya nchi wanaosajiliwa hapa nchini ni lazima wawe na ubora pamoja na viwango vinavyotakiwa.
 
Akifafanua suala hilo Bw. Singo amesema kuwa michezo yote ya kulipwa kwa sasa imeendelea kukua duniani kote na nchi yetu pia inayo wachezaji wengi wanaocheza michezo hii ikiwemo Mpira wa Kikapu (Basketball), Kriketi, Mpira wa Miguu na michezo mingine, hivyo, Serikali haijatoa maelekezo ya ukomo wa usajili wa idadi ya wachezaji bali inataka kuwepo kwa mjadala wa wazi utakaotoa mwongozo wa ukomo wa idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni.
 
Aidha, Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wadau wa michezo nchini watakapopata fursa ya kuchangia au kutoa maoni katika mjadala huo wasiegemee katika timu wanazoshabikia, bali watoe maoni ambayo yatasaidia kuendeleza michezo na kuendeleza vipaji vya wanamichezo wetu pamoja na kukuza michezo nchini.
MWISHO






from MPEKUZI

Comments