Katika hali ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona, Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka maafisa uhamiaji pamoja na watumishi wengine katika bandari za mkoa huo pamoja na mpaka wa nchi kavu kuacha tabia ya kupokea rushwa kutoka kwa wageni hasa katika kipindi hiki ambacho ni hatari kwa nchi.
Mh. Wangabo amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa kwani kuwapitisha wageni hao kwa kutumia rushwa kutasababisha nchi itaingia kwenye madhara makubwa ikiwemo kuliangamiza taifa na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni sawa na usaliti kwa nchi, hivyo aliwataka watumishi hao kuwa wazalendo na nchi yao, kwani kutofanya hivyo kuna uwezekano wa kupitisha mgonjwa mmoja ambae ataweza kupelekea madhara makubwa katika nchi.
“Kwahiyo muwe makini sana, vitendo vya rushwa marufuku na kila jambo lichukuliwe kwa umuhimu na uzito mkubwa sana, kumbukeni kwamba kwenye mipaka ndipo mmebeba taifa, kwasababu atakayepitishwa pale bila ya kuzingatia taratibu zinazotakiwa, bila ya kuchunguzwa vizuri, bila ya kuulizwa ulizwa vizuri historia alikotokea na kumuweka katika “isolation room” kama itabidi kulingana na atakavyokuwa ameonekana, msipofanya hivyo mtu akapita, basi mjue kabisa kwamba analeta vifo katika nchi yet una huo utakuwa ni usaliti kwasababu umelisaliti taifa kwa kupitisha mtu ili aje atuue,” alisisitiza.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea katika bandari ya Kabwe iliyopo katika kata ya Kabwe, Wilayani Nkasi ili kukagua utekelezaji wa maelekezo ya serikali juu ya kuandaa maeneo maalumu kwaajili ya kuwaweka wageni kwa siku 14 pamoja na kuona kituo cha huduma ya afya kilichotengwa maalum kwaajili ya kuwapokea watu wanaodhaniwa kuwa na ugonjwa wa Corona kwa uangalizi zaidi ambapo katika ziara hiyo aliambatana na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa pamoja na wataalamu wengine.
Aidha, Mh. Wangabo ameutaka uongozi wa Wilaya kuhakikisha wanatoa elimu ya udhibiti wa ugonjwa wa Corona kwa wenyeviti wa vijiji vyote vilivyopo katika mwambao wa ziwa Tanganyika kwani imebainika kuwa mara kadhaa vijiji hivyo hutumika kama bandari zisizo rasmi kuingiza wageni wanaotoka katika nchi za Jamhuri ya Watu wa Kongo, Burundi pamoja na Zambia.
Wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo wa Corona Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Dkt. Hashim Mvogogo amesema kuwa majengo ya Hospitali ya Wilaya yamepangwa kutumika kuhifadhi wagonjwa watakaobainika kuwa na Virusi vya Corona baada ya siku 14 na pia kutumika kama kituo cha tiba endapo wagonjwa hao watatokea na kuongezeka na kuongeza kuwa kata 21 na vijiji 62 vimeshapewa elimu ya afaya ya kujikinga na ugonjwa huo huku wananchi wakionekana kuelewa na kuhamasika.
“Katika Kata tumetumia wasimamizi wa afya, ndio maana ukiangalia hata katika baadhi ya shule kabla hazijafungwa tulizifikia shule 42, kwahiyo tulianza “intervention” mapema kwa maana ile timu ya Wilaya hatukuweza kufika kwenye hizo sehemu lakini tulitumia wataalamu wetu ambao wako katika zile sehemu, kwahiyo kiujumla kama elimu kiwilaya wote, karibia kata zote wanahiyo elimu, lakini zile kata ambazo hatukufikia wataalamu kutoka ngazi ya wilaya, tunahitaji pia tuzifikie na sisi,” Alisema.
Kwa upande wake Mwangalizi wa Bandari ya Kabwe Mohamed Issa amesema kuwa mbali na kutenga nyumba mojawapo ya mtumishi kwaajili ya kuwahifadhi wageni watakaoingia nchini kwa siku 14, pia kuna boti maalum ambayo imeandaliwa kwaajili ya kufanya doria katika badari bubu zaidi ya nne zilizopo katika vya karibu na bandari hiyo ili kujihadhari na uingiaji holela wa wageni hao.
“Boti hii ni kwaajili ya kufanya “patrol” kwenye bandari bubu ambazo ni pamoja na Utinta, Kalila, Korongwe na Msalamba ndio bandari bubu ambazo zinatumiwa na wafanyabiashara ambao sio waaminifu wanaokwepa mapato ya serikali, kwahiyo hii boti itatusaidia kufika maeneo hayo kwa urahisi ili pia kulinda mapato ya serikali,” Alisema.
Katika Wilaya ya Nkasi kuna bandari bubu zaidi ya 12 ambazo hutumika na wageni kuingia nchini huku bandari rasmi zinaz otambulika ni 3 ikiwemo, Kirando, Kabwe na Wampembe ambapo bandari hiyo ya ipo katika hatua za mwisho kumalizika kutanuliwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 7.4 na ujenzi wake kufikia asilimia 95% hali iliyopelekea Mh. Wangabo kuwataka wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuitumia bandari hiyo na fursa zake vizuri ili kujiingizia kipato.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment