TAKUKURU mkoani Dodoma Yamnasa Kaimu Katibu Tume Ya Utumishi Kwa Kuomba Rushwa

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa [TAKUKURU]Mkoa wa Dodoma inatarajia kumfikisha  katika mahakama ya Wilaya ya Bahi Kaimu katibu wa Tume ya utumishi wilayani hapo Bw.Adam Israel Richard [49] na kumfungulia mashauri manne ya kuomba Jumla ya Tsh.Milioni moja na elfu hamsini[1,050,000]na kupokea Tsh.laki tano na Tsh.elfu hamsini na tatu[553,000] kutoka kwa walimu wanne ili awasaidie katika mchakato wa kupandishwa  madaraja ama au vyeo.

Akizungumza na Waandishi wa habari  hapo jana  Machi 25,2020 jijini Dodoma,mkuu wa TAKUKURU mkoani hapa Bw.Sosthenes Kibwengo alisema hiyo ni kinyume na kifungu cha 15 [1]cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  sura ya 329  marejeo ya mwaka 2018 .

“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa walimu kwamba mtuhumiwa  ana tabia ya kutumia rushwa kama kigezo cha kufanikisha  waliompa kupandishwa madaraja ,tulianzisha uchunguzi  na tumepata ushahidi kwamba kati ya April,na Juni,2019  mtuhumiwa alitenda kosa hilo na kwa kuwa taarifa tulizopata dhidi yake ni nyingi ,bado uchunguzi wa taarifa zilizosalia unaendelea na ukikamilika atafikishwa mahakamani”alisema.

Aidha,Bw.Kibwengo alisema TAKUKURU imemfikisha mahakama ya Wilaya ya Kondoa  Afisa mtendaji kata ya Thawi Wilayani hapo   Bw.Hashim Ally Mohamed [42] na kumfungulia kesi mbili  kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa  ambapo amefunguliwa  shauri la jinai Na.24/2020 mbele ya Hakimu Mwajabu Mvungi .

Bw.Kibwengo alifafanua kuwa mtuhumiwa alifanya kosa la kuomba Rushwa  ya Tsh.laki moja na elfu hamsini na tano [155,000] na kupokea Tsh.elfu sitini[60,000] kutoka kwa mwananchi mmoja  ili asimchukulie hatua kwa kosa la mjukuu wa mwananchi huyo  kutokwenda shule kwa siku thelathini na moja[31]mfululizo .

“Uchunguzi wetu pia umeonesha kuwa mwanafunzi huyo alifuata taratibu zote   na amehamia katika shule iliyopo mkoa mwingine ,pili amefunguliwa shauri la jinai Na.26/2020 Mbele ya Hakimu Martine  Massao  kwa kosa la kuomba rushwa  Tsh.laki moja na elfu sabini na tano[1,75,000] na kupokea Tsh.elfu themanini[80,000] kutoka kwa mwananchi mwingine  ili asichukue hatua dhidi yake kwa madai kwamba binti yake hajahudhuria masomo shuleni na alitenda vitendo hivyo vya jinai Februari mwaka huu”alisema Kibwengo.

Katika hatua nyingine Bw.Kibwengo amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa wanatarajia kumfikisha mahakamani Dodoma mwalimu mkuu wa shule ya msingi  Msisi ya jijini hapa  Bw.David Isaac Mdeka[44] mkazi wa Ipagala kwa makosa ya matumizi ya nyaraka  kumdanganya mwajiri  kinyume na kifungu cha 22 na ubadhirifu  kinyume na kifungu cha 28  ,vyote vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa  na kosa la kughushi  kinyume na sheria za kanuni za Adhabu   Sura ya 16 marejeo ya Mwaka 2002.

“Uchunguzi wetu  umeonesha kwamba Januari ,2015  mtuhumiwa akiwa katibu wa kamati ya shule  alighushi mhutasari  kuonesha kwamba kamati imeridhia malipo ya Tsh.Milioni moja ,laki moja nan a elfu themanini na sita [1,186,000] kwa ajili ya kununua vifaa vya kukarabati choo cha shule ,ambapo alitoa fedha hizo benki  na kuzifuja  kwani vifaa havikufikishwa shuleni  na wala ukarabati haukufanyika “amesema.

Pia Bw.Kibwengo alisema wanashirikiana na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa  kuwafikisha mahakamani Dodoma Bw.Robert Daniel Mwinje [39]na Bi.Nyemo Msafiri Malenda [20]wote wakazi wa jijini Dodoma kwa makosa matatu ya kula njama ,kughushi, na kuwasilisha nyaraka za uongo ,yote yakiwa ni kinyume cha sheria  ya kanuni za Adhabu  Sura ya 16 marejeo yam waka 2018.

“Uchunguzi wetu umeonesha kwamba kati ya tarehe 18  na 20 ,Oktoba,2019,Bw.Mwinje ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma na Bi.Malenda ambaye ni mhudumu wa Ofisi hiyo walighushi  barua ya uteuzi wa waomba uongozi  ndani ya Chama  na huku wakijifanya  imetolewa na uongozi wa Chama cha Mapinduzi  wilaya ya Dodoma  wakaikabidhi kwa uongozi wa mwanachama mmoja  kwa hatua huku wakijua kuwa ni uongo”alisema Bw.Kibwengo.

Sanjari na hayo Bw.Kibwengo alisema TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imeendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa  kwa kuwashirikisha wananchi huku akiwashukuru kwa kutoa ushirikiano  na kuwasihi watumishi wa umma kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu za utumishi  kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki .


from MPEKUZI

Comments