Naibu Waziri Mabula Aridhishwa Na Kasi Ya Ujenzi Hospitali Ya Rufaa Mkoa Wa Mara

Na Munir Shemweta, WANMM, MUSOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoko Kwangwa Musoma unaogharimu takriban Bilioni 15.082.

Dkt Mabula aliridhishwa na kasi ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo alipokwenda kukagua maendeleo ya ujezi wake jana wakati akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Mara.

Alisema, ujenzi wa mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa Mara sambamba na mikoa na nchi jirani kwa kuwa itakuwa ikitoa huduma za kitabibu kwa wananchi wa maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alibainisha kuwa, hana mashaka na Shirika la Nyumba la Taifa katika kutekeleza mradi huo kutokana na Shirika hilo kufanya vizuri kwenye miradi mbalimbali inayosimamia.

‘’Kwa sasa sina mashaka na Shirika la Nyumba la Taifa katika masuala ya ujenzi kutokana na kufanya vizuri kwenye miradi mingi ya ujenzi inayosimamia lakini kinachotakiwa hapa ni kukamilisha ujenzi kwa wakati’’ alisema Dkt Mabula

Ameitaja baadhi ya miradi ya ujenzi inayofanywa na NHC na kufanya vizuri kwenye maeneo mablimbali kuwa ni ujenzi wa ofisi kumi na saba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),  Hospitali ya Rufaa ya Kusini iliyopo Mtwara, Ofisi ya wilaya ya Wang’ingombe na nyumba za wakuu wa wilaya za Hai na Ulanga.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mara Goodluck Thomas alisema Shirika lake katika kutekeleza mradi huo tayari baadhi ya kazi zimekamilishwa ikiwemo jengo la Huduma ya Mama na Mtoto, nyongeza ya ghorofa moja na kupaua, kupiga plaster nje na ndani, maandalizi ya rangi, fremu za milango pamoja na kuweka marumaru.

Kwa mujibu wa Goodluck, kazi zinazoendelea sasa ni uwekaji mifumo ya maji safi na maji taka, kazi ya umeme, uwekaji mifumo ya gesi, ufungaji madirisha ya alminiuam na ukamilishaji kazi nyingine ukiendelea na mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo umefikia asilimia 65.

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt Vincent Naano Anney alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa wakati ujenzi wa hospitali hiyo ukiendelea kukamilishwa kuna haja kwa mamlaka husika  kuanza kuangalia mahitaji ya Wataalamu na Vifaa vinavyohitajika kwenye vitengo mbalimbali vya hospitali hiyo na kubainisha kuwa kazi hiyo isipofanyika mapema kuna hatari ujenzi utakapokamilika hospitali hiyo ikakosa wataalamu wa kutosha kutokana na ukubwa wake.


from MPEKUZI

Comments