Mke na Mume Watiwa Mbaroni Kwa Kutoa Taarifa za Uongo Kuhusu Corona

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linawashikilia watu wawili ambao ni mume na mke kwa tuhuma na kueneza taarifa za uongo kwa wananchi kuhusu ugonjwa COVID-19(Corona) na kwamba watafikishwa mahakamani wakati wowote.

Akizungumza leo  Machi 27 mwaka 2020 ,Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema watu hao wamekamatwa Machi 20 mwaka huu saa saba mchana  wakiwa kwenye daladala aina ya Toyota DCM namba T 119 DKS iliyokuwa ikitokea Muhimbili.


“Tunawashikilia watuhumiwa wawili Boniphace Mwita na Mkewe Rosemary wakazi wa Tabata,DSM kwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu corona wakiwa kwenye daladala ambapo walianza kupotosha, kukejeli na kutania kwa kusema Serikali inapotosha Wananchi kwamba kuna corona”-Amesema Mambosasa.

Kamanda Mambosasa amesema kuwa kutokana na kejeli na uzushi wa watu hao abiria waliokuwepo ndani ya daladala hiyo walikasirishwa na kuchukua hatua za kuwaweka chini ya ulinzi na  kuitaka daladala hiyo ipelekwe Kituo cha Polisi na sasa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya hatua inayofuata ya kuwapeleka mahakamani.

“Baada ya Mwita na Mkewe kusema Serikali inapotosha kuhusu corona na haina fedha ndio maana imefunga shule na vyuo kwa kisingizio cha corona, abiria ktk daladala iliwakera wakawaweka chini ya ulinzi wakamuamuru Dereva apeleke gari Polisi, tunao, tutawapeleka Mahakamani”-Mambosasa


Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi limeshachukua maelezo ya watuhumiwa hao na jarada tayari wameshapeleka kwa Wakili wa Serikali kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.


from MPEKUZI

Comments