Idadi Ya Maambuki ya Corona Nchini Kenya Yafika 42


Watu wanne zaidi wameambukizwa virusi vya Corona nchini Kenya na kufikisha idadi ya wagonjwa kufikia 42, wakati huu serikali nchini humo ikiendelea kutekeleza amri ya watu kutotoka nje, ambayo imeathiri shughuli za biashara .

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema kuwa watatu walioambukizwa ni raia wa Marekani, Cameroon na Burkina Faso, huku mmoja akiwa raia wa Kenya.

Maambukizi matatu yameripotiwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi na moja jijini Mombasa. watu 1,426 waliotangamana na ambao wanashukiwa kuambukizwa virusi hivyo wanatafutwa.

Hata hivyo wataalamu wa afya wanasema licha ya mikakati muhimu iliyotangazwa na Serikali kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, vita ya kuukabili itakuwa ngumu ikiwa wananchi hawataendelea kuelimishwa kuzingatia usafi na njia za kujikinga.

Kenya kwa sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwatafuta watu waliotangamana na watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Covid-19.

Hivi karibuni msemaji wa serikali, Cyrus Oguna, alitoa wito kwa watu ambao huenda walitangamana na wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo kufika katika kituo cha afya kilicho karibu nao.


from MPEKUZI

Comments