Wananchi Washauriwa Kutochakaza Noti Na Sarafu

Gavana  wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) Profesa. Frolens Luoga amewashauri wananchi kutumia vyema fedha bila kuziharibu wala kuzichakaza kutokana na ubora na uthamani wa utengenezaji wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Prof. Luoga amesema, lazima fedha zitumike kwa uangalifu na kuwaasa wananchi kutumia fedha hizo bila kuzichakaza, kuzitupa wala kuziandika kwa kuwa fedha hizo zinapoharibiwa zinakuwa katika hatari ya kuharibiwa kabisa na mashine maalumu pindi zinapofika benki kuu, na kupelekea gharama ya kupata nyingine kupata fedha hiyo.

Profesa. Luoga amesema kuwa mabenki yana wajibu wa kusaidia benki kuu katika kutekeleza Sera ya Sarafu safi kwa kukusanya pesa zote zilizochafuka na zisizo na hali nzuri na kuzirudisha  benki kuu.

Amesema kuwa fedha ya nchi ina thamani kubwa hivyo lazima matumizi yake yawe ya uangalifu,

"Noti ya Tanzania inatengenezwa kwa gharama zaidi kwani inatengenezwa kwa pamba kwa asilimia 100 ukilinganisha na noti ya dola ambayo hutengenezwa kwa pamba kwa asilimia 75 ya pamba, na hiyo ni kutokana na matumizi" amesema.

Pia amesema kuwa Benki kuu itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kuwawajibisha wale wote watakaokutwa na hatia ya kuharibu pesa ambalo ni kosa la jinai.

"Kuchana noti ni kosa la jinai, wengi wamekuwa wakija benki kudanganya ili walipwe tumewabaini walioghushi na waliokamatwa wanachukulia sheria kwa kuwa hiyo sio biashara" Ameeleza Prof. Luoga.

Kuhusiana na malalamiko ya kupungua kwa pesa katika mzunguko Gavana huyo ameeleza kuwa;

" Kila asubuhi tunakutana na kuangaalia hali ya ukwasi katika mabenki na tunajua kila benki ina kiasi gani na tunaweza kutoa mkopo kwa mabenki ili waweze kufanya malipo" ameeleza

Amesema kuwa "Benki kuu inaangalia kiasi cha pesa katika  mabenki yote na kama benki haitakua na pesa tutaangalia ni kwanini na tutasaidia na ikitokea benki haina pesa kwa kutokidhi masharti kama benki tunachukua hatua nyingine" amesema Luoga.

Mwisho amewataka wananchi kutoghushi pesa ya nchi na kwa yeyote atakayekutwa na pesa bandia  atashtakiwa kwa  kosa la jinai na uhujumu uchumi.


from MPEKUZI

Comments