Waitara atangaza kugombea ubunge Tarime Vijijini

Mbunge wa Ukonga, Dar es Salaam, Mwita Waitara (CCM), ametangaza kugombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara.

Waitara ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), aliyejichimbia kwa muda akifanya vikao ndani na mikutano ya hadhara, alitangaza uamuzi wake huo hivi karibuni wilayani Tarime alipokutana na viongozi wa chama na jumuiya, wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuanzia ngazi ya mashina, matawi na kata.

Aliwaeleza wajumbe hao zaidi ya 700 kuwa ameamua kurudi nyumbani kugombea, huku akitamba yeye ndiye mtu pekee ndani ya CCM mwenye uwezo na nguvu za kukomboa jimbo hilo kutoka Chadema.

Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na John Heche (Chadema) aliyeshinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Niseme nisiseme au kuna mtu atanuna humu ndani, si mnajua nakuja nyumbani au ngoja niseme tu, naogopa nini, mie nagombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini, mchakato utafanyika wa kura za maoni, kisha utaratibu wa vikao vya wilaya utapitia.

“Itafikia hatua ya mkoa na mwisho vikao vya juu vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kuteua jina moja ambalo ni la Waitara, kisha NEC wanatuunganisha na upinzani kuanza kampeni za miezi mitatu kabla wananchi kutupigia kura Oktoba, mwaka huu,” alisema Waitara.

Waitara ameendelea kufanya vikao vya kukutana na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya, akitumia ushawishi wa kutoa ahadi kedekede, kuwapatia nauli na wakati mwingine kuchinja mifugo na kuandaa chakula na vinywaji baridi, akidai ni sehemu ya kubadilishana mawazo na kuweka mikakati ya kuunda timu ya watu watakaomsaidia kumtafutia kura kwa wajumbe wa mkutano mkuu ili kumuwezesha kuibuka mshindi wa kura za maoni ndani ya chama hicho.


from MPEKUZI

Comments