Vijana Wenye Nia Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo Waahidiwa Kupewa Ardhi Songwe

Vijana wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo Mkoani Songwe wamepewa ahadi ya kupatiwa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo ndani ya muda mfupi baada ya kuwasilisha maombi yao.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amtoa ahadi hiyo leo wakati akifunga Kongamano la Vijana  katika Kilimo lililofanyika Mkoa wa Songwe na Kuhusisha vijana takribani 700 kutoka Mikoa ya Songwe, Rukwa, Mbeya na Katavi.

Brig. Jen. Mwangela amesema Mkoa wa Songwe unayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya shughuli za Kilimo ambayo bado haijatumika hivyo kijana yeyote mwenye nia ya kuwekeza katika Kilimo afike ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

“Mkoa una hekta Milioni mbili, mpaka sasa tumetumia asilimia 30 kwa ajili ya kilimo na asilimia ndogo kwa ajili ya makazi na misitu hivyo tunalo eneo la kutosha, mvua za kutosha na ardhi nzuri pia tunazo hekta elfu 18 zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha umwgiliaji hivyo ardhi bado ipo ya kutosha.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.

Ameongeza kuwa kijana mwenye nia ya kuwekeza kwenye Kilimo akifika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ata taja Wilaya anayotaka kewekeza ili aelekezwe isipokuwa kijana hatatakiwa kuchagua mwenyewe eneo maalumu ambalo tayari linamilikiwa na watu wengine.

Brig. Jen. Mwangela amewasisitiza Vijana kuchangamkia fursa ya kumiliki ardhi kihalali kwakuwa bado inapatikana kwa urahisi ili baadaye wasihangaike kuitafuta wakati wa uzee na kuongeza kuwa waache kulalamikia wazazi au serikali kutokana na umasikini bali wajikite katika Kilimo.

Amesema asilimia 67 ya nguvu kazi ni vijana ambao hawana ajira ambapo nguvu kazi hii ikibaki bila ajira ni aibu kwa vijana na taifa hivyo mkakati wa Wizara ya Kilimo wa Kuhakikisha vijana wanajikita katika Kilimo ni mzuri na utainua uchumi wa taifa kwa haraka.

Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa vijana wakishiriki kikamilifu katika Kilimo uchumi utakua, viwanda vitaongezeka na wataweza kuyafurahia maisha kwakuwa Kilimo hakijawahi kumtupa mtu na pia wasiache kuangalia fursa katika sekta za ufugaji na uvuvi.

Aidha Brig. Jen. Mwangela amewaeleza Vijana waliohudhuria Kongamano hilo kuwa Serikali itawaunganisha na taasisi zinazotoa mikopo ya Kilimo isipokuwa watatakiwa kuwa waamini na kurejesha mikopo hiyo.

Ameongeza kuwa wapo baadhi ya watu ambao walipatiwa mikopo ya Kilimo na baadhi ya benki lakini wamekuwa sio waaminifu kwa kutorudisha mikopo hiyo au kuwa wasumbufu katika kurejesha mikopo hiyo hivyo vijana hao wasiige mifano yao.

 Naye Afisa Programu kutoka Jukwa la Wadau wa Kilimo (ANSAF) Rehema Msami amesema wamefanya utafiti kuhusu namna ambayo halmashauri zimekuwa zikitoa asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu.

Msami amesema utafiti wao umebaini kuwa vijana wengi wenye sifa hawapati mikopo hiyo na hivyo kushindwa kuwa na mitaji ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, pia baadhi ya vijana wanaopewa mikopo hawana sifa na hivyo kushindwa kurejesha mikopo hiyo.

Nelusigwe Kibona kijana Mkulima wa Mbogamboga kutoka Rungwe Mkoani Mbeya amesema Kongamano la Vijana limempa elimu na mbinu nyingi za Kulima kisasa pamoja na kutafuta masoko ya mazao yake.

Kibona ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Songwe kwa kuwasaidia vijana kupata ardhi kwa ajili ya Kilimo na kuiomba mikoa mingine iige mfano huo.

Kenedy Kyando Kijana Mkulima Kutoka Vwawa Songwe amesema kuwa Vijana wengi hawataki kujishughulisha na Kilimo kwa kukosa uvumilivu na kutaka fedha za haraka huku akiiomba Serikali kufanya makongamano kama hayo mara kwa mara.


from MPEKUZI

Comments