TAHARUKI kubwa imeibuka kwa wananchi wa Kijiji cha Ngiresi kilichopo kwenye Kata ya Sokoni 2 katika Halmashauri ya Arusha baada kuzaliwa ng'ombe mwenye vichwa viwili ,midomo miwili na macho matatu .
Kuzaliwa kwa ng'ombe huyo katika eneo hilo kumeibua maswali mengi yasiyo na majibu kwa wananchi hao huku wengi wao wakionekana kushangaa.
Akizungumzia tukio hilo, Mmiliki wa ng'ombe huyo Eliakimu Mungasi amesema kwamba wakati anapewa taarifa ya kuzaliwa kwa ng'ombe huyo alipata mshutuko mkubwa kwani haijawahi kutokea katika maisha yake na kwamba ng'ombe huyo amezaliwa Februari 3 mwaka huu na hadi sasa ametimiza siku 23.
Amesema huu ni uzao wa tano wa ng'ombe aliyezaa ndama huyo ambaye amewashangaza wengi na kwamba huko nyuma ng'ombe wote waliozaliwa walikuwa salama na hawana tatizo lolote.
"Watu wanaongea mengi, wengine wanasema ni mambo ya ushirikina kwa maana ya uchawi, wengine wanasema ni laana lakini mimi sijali, nachojua ni mpango wa Mungu na tutaendelea kumtunza,"amesema Mungasi
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Halmashaur ya Arusha Arusha Charles Ngiroriti amesema hali hiyo ni kawaida kutokea kwa wanyama.Katika utungaji wa kiumbe inaweza ikatokea cell zikagawanyika ,kama vile zilitaka kutengeneza viumbe viwili.
Ameongeza lakini zikishindwa kigawanyika na kufika mwisho ndio anatokea kiumbe wa aina hiyo na kwamba hali hiyo haiuhusiani na imani za kishirikina, hivyo watu waache kuzusha maneno.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment