Mganga Wa Kienyeji Ahukumiwa Kifungo Cha Maisha Jela Kwa Kumbaka Mtoto wa Miaka 8

Mahakama ya Wilaya Kigoma Mkoa wa Kigoma imemhukumu mganga wa kienyeji, Venas Edward (48), mkazi wa Ujiji Manispaa ya Kigoma/Ujiji kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumnajisi mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Katoki Mwakitalu, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka yoyote.

Hakimu Mwakitalu alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Raymond Kimbe, na ulipeleka mashahidi wanne na kielelezo kimoja ambacho ni PF3.

Alisema mama wa mtoto huyo alimpeleka mtoto wake nyumbani kwa mshtakiwa kwa ajili ya kutibiwa, na baada ya kumfikisha, mganga alimtuma mama huyo aende dukani kununua wembe.

Alisema baada ya mama kwenda dukani, mshtakiwa alimfanyia mtoto huyo kitendo hucho cha kikatili.

Alieleza kuwa baadaye mama wa mtoto huyo alifika kutoka dukani na kumchukua mtoto wake na kurudi nyumbani kwake.

Alieleza zaidi kuwa baada ya muda mama alisikia mtoto wake analalamika kusikia maumivu sehemu zake za siri, ndipo mama alipomkagua na kugundua kuwa mtoto wake alikuwa amenajisiwa.

Aliendelea kueleza kuwa mama wa mtoto huyo alimbana mtoto wake kwa kumuuliza ni nani aliyekufanyia kitendo hicho ndipo alimjibu kuwa ni mshtakiwa.

Mshtakiwa huyo baada ya kuhukumiwa kwenda jela maisha, aliangua kilio hadharani na kusababisha ndugu zake nao kuanza kuangua vilio mahakamani mbele ya umati uliofika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza hukumu hiyo.

Awali akisoma hati ya mashtaka Wakili Kimbe alidai kuwa Aprili 23, mwaka 2019 majira ya asubuhi eneo la Kasoko Ujiji, mshtakiwa alinajisi mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.


from MPEKUZI

Comments