Serikali imesema kuwa endapo mbunge ataona kuwa kuna haja ya kubadilishwa sheria ya makosa ya uhujumu uchumi ili watuhumiwa wa makosa hayo yawe na dhamana awasilishe hoja yake bungeni kwani Bunge ndiyo chombo chenye mamlaka ya kutunga na kubadili sheria.
Hayo yamesemwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandishi Hamad Masauni wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika kikao cha pili cha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Sabreena Hamza Sungura.
Katika swali lake mbunge huyo aliuliza, “Kutokana na msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani, Je! Serikali haioni ni muda muafaka sasa wa kubadili sheria hiyo ili majaji waweze kutoa dhamana kwa watuhumiwa, kwani kwa hali ilivyo sasa hata mtu anayetuhumiwa kuhujumu Tsh 20,000 ananyimwa dhamana?
“Ni mamlaka ya Bunge hili kutunga sheria na kubadilisha pale unapoona inafaa, na yeye ni mbunge wa Bunge hili na kanuni anazifahamu. Kama anaona kuna utaratibu unaofaa (kubadili sheria), ni haki ya mbunge kutumia haki yake ya kikanuni,” ameeleza Masauni.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania kwa sasa, mtu akishtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi, mahakama haina mamlaka ya kumpa dhamana, na kwamba atakaa rumande hadi hapo hukumu ya kesi itakapotolewa ama aachiwe huru au apewe adhabu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment