Waziri Mkuu Aagiza Miundombinu Ya Shule Ikamilike Mapema....Asema Kama kuna wahusika walioko likizo warudishwe haraka

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya shule ikamilike mapema na kama kuna watendaji walioko likizo warudi kwani Serikali inataka wanafunzi wote waanze masomo pamoja.

Ameyasema hayo jana (Jumanne, Desemba 31, 2019) wakati alipofanya ziara kukagua ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleoa wilayani Ruangwa. Amesisitiza ukamilishwaji wa miradi hiyo ili wananchi waanze kuitumia.

Waziri Mkuu amesema agizo alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Desemba 29, 2019 kuhusu usimamizi wa miundimbinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa liko pale pale kwa sababu Serikali haitaki kuona wanafunzi wakipishana katika kuanza masomo.

Miradi ambayo Waziri Mkuu ameitembelea ni ujenzi wa shule ya msingi ya Ng’au ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, ujenzi wa chuo cha VETA, hospitali ya wilaya ya Ruangwa na shule ya sekondari ya Lucas Maria.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo hivyo ni lazima viongozi katika maeneo husika wahakikishe wanashirikiana katika kusimamia utekelezaji wake.

Amesema wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020, hivyo ni lazima usimamizi ukaongezwa katika baadhi ya maeneo ambayo miundombinu yake bado haijakamilika ili kuwahi masomo.

Akiwa katika shule ya Sekondari ya Lucas Maria Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Andrea Chezue ahakikishe mafundi wanafanya kazi usiku na mchana.

“Shule zinakaribia kufunguliwa na baadhi ya majengo kama bwalo, maabara, nyumba za walimu hayajakamilika mafundi hawapo eneo la ujenzi na Serikali imetoa fedha. Nataka kazi hii ikamilike mapema kwani hakuna sababu.”

Wakati huo huo, Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa wamepongeza na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wananchi hao wakiwemo vijana wanaojenga chuo cha VETA walitoa pongezi na shukrani hizo mbele ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza kukagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho. Mafunzo yatakayotolewa chuoni hapo ni pamoja na ufundi uashi, seremala, magari, ushonaji nguo na Tehama.

Kadhalika, vijana hao wamewashauri vijana wenzao wajitokeze na kuchangamkia fursa za ajira zinazopatikana katika maeneo yao kupitia miradi mbalimbali inayotokelezwa na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi.


from MPEKUZI

Comments