Waziri Kalemani Aagiza Kuwekwa Ndani Wakandarasi Wa Umeme Vijiji Kigoma

Hafsa omar-Kigoma
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi. Mwanamvua Mrindoko kuwaweka ndani na kuwanyang’anya pasipoti zao, wakandarasi wa kampuni ya ETERN-CCCE waliopewa kazi ya kusambaza umeme vijijini baada ya kusuasua katika utekelezaji wa kazi.

Alitoa agizo hilo Desemba 22,2019, akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nguruka, Wilaya ya Uvinza, Mkoani Kigoma, katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme mkoani humo.

Aidha, alisema amechukua hatua hiyo mara baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme Mkoani humo na kuona maeneo mengi yakiwa bado hayajasambaziwa umeme kutokana na kusuasu katika kazi kwa mkandarasi huyo.

“ Wameanza kazi lakini spidi yao ni ya kusuasua sana, spidi yao hairidhishi huo ndio ukweli, lakini hatuwezi kubaki tunalalamika lazima tuanze kuchukua hatua, leo nimekuja kukagua hapa nimekuta amewasha vijiji saba tu ambapo zaidi ya vijiji hamsini bado havijawashwa ” alisema.

Dkt. Kalemani, pia alichukizwa na kitendo cha wakandarasi hao kufanya kazi kwa udanganyifu kwa kuweka nguzo na transfoma katika eneo hilo siku moja kabda ya ziara yake kijijini humo, na kuwataka wakandarasi hao kufanya kwa mujibu wa mkataba.

Vile vile, aliwagiza wakandarasi hao ifikapo januari 10 mwakani wawe tayari wamewasha umeme katika kijiji hicho na Vitongoji vyake vyote na kuongeza spidi ya kufanya kazi pamoja kuajiri vibarua wengi ili kasi ya usambazaji umeme iongezeke.

Katika ziara yake mkoani humo, Waziri wa Nishati, alikagua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nguruka, kituo ambacho kikikamilika Mkoa wa Kigoma utaunganishwa na gridi ya taifa.


from MPEKUZI

Comments