Trump apandwa na hasira Baada Ya Waandamanaji Kuuvamia ubalozi wa Marekani nchini Iraq na Kutaka Kuuchoma Moto

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema anatarajia Iraq itatumia vikosi vyake vya usalama kuulinda ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.

Kauli hiyo ameitoa wakati ambapo anailaumu Iran kwa kuchochea vurugu hizo dhidi ya eneo lake. 

Wananchi wa Iraq ambao ni wafuasi wa wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran waliandamana kwenye ubalozi wa Marekani siku ya Jumanne huku wakiimba nyimbo zinazosema ''Kifo cha Marekani,'' wakirusha mawe, wakivunja kamera za usalama pamoja na kulichoma moto eneo la mapokezi, wakilaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani.

Mashambulizi hayo yaliyofanyika Jumapili iliyopita yaliwaua wapiganaji wapatao 25 wa kundi la wanamgambo wa Kataeb Hezbollah. 

''Tunatarajia Iraq itavitumia vikosi vyake kuulinda ubalozi na tumearifiwa hivyo,'' ameandika Trump katika ukurasa wake wa Twitter. Trump amesema Iran itawajibika kikamilifu kwa machafuko hayo.

Mashambulizi ya Marekani yalikuwa ni kujibu shambulizi la roketi lililofanywa wiki iliyopita na kumuua mkandarasi mmoja wa Kimarekani katika kituo cha jeshi la Iraq, ambalo ni la karibuni kufnayika lililenga maslahi ya Marekani nchini Iraq. 

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulizi hilo, lakini vikosi vya usalama vya Marekani vimelishutumu kundi la Kataeb Hezbollah.
 
Trump amesema Marekani imejibu vikali shambulizi ambalo limemuua mkandarasi huyo na skwamba siku zote itafanya hivyo. 

Uhusiano kati ya Marekani na Iran umekuwa ukizorota tangu Marekani ilivyojiondoa kwenye mkataba wa kihistoria wa nyuklia wa Iran mwaka 2018 na kuweka vikwazo vipya.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kadhaa kwa waandamanaji kufanikiwa kuufikia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, uliopo kwenye eneo lenye ulinzi mkali maarufu kama Green Zone. 

Vikosi vya usalama ndani ya ubalozi huo walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji nje ya ubalozi huo. Imeripotiwa kuwa zaidi ya watu 20,000 walikusanyika nje ya ubalozi huo.


from MPEKUZI

Comments