Tito Magoti na Wenzake Wapandishwa Kizimbani Kwa Uhujumu Uchumi na Kutakatisha Fedha

Mfanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania, Tito Magoti (26) na Theodory Giyani (36), wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi  likiwamo la utakatishaji fedha kiasi cha Sh17milioni.

Magoti na mwenzake Theodory Giyan ambaye nii Mtaalamu wa TEHAMA wamefikishwa Kisutu na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Janeth Mtega na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi,Faraja Nchimbi na Renatus  Mkude.

Kabla ya kusomewa mashtaka hao, hakimu Mtega amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP).

Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai Magoti na Giyani, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 137/2019.

Simon alidai katika shtaka la kwanza, Magoti na Giyani wanadaiwa kushiriki genge la uhalifu.

Amedai Tito na mwenzake katika tarehe tofauti February Mosi - Dec 17,2019 ndani ya DSM na maeneo mengine ya Tanzania, wakishirikiana na watu ambao hawapo Mahakamani kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai katika shtaka la pili, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, wanadaiwa siku na eneo hilo, wanadaiwa kumiliki  programu za kompyuta kwa lengo la kutenda kosa la uhalifu.

Katika shtaka la tatu, ambalo ni kutakatisha fedha, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, alidai Magoti na Giyani, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya nchi.

Wanashtakiwa hao wanadaiwa katika tarehe hizo, walijipatia Sh17.35 milioni wakati wakijua fedha hizo ni zao tangulizi la kushiriki genge la uhalifu.

Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2020 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande


from MPEKUZI

Comments