Mkurugenzi wa Shule za Zam Zam Akutwa Amefariki Ofisini Kwake

Mkurugenzi wa Shule za Zam Zam jijini Dodoma  Sheikh Rashid Bura amekutwa amefariki dunia ofisini kwake eneo la Majani ya Chai karibu na Nyerere square jijini humo.

Bura aliondoka nyumbani kwake zaidi ya siku nne zilizopita na hakujulikani alipokwenda ambapo juhudi za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio hadi jana Jumatano Desemba 25, 2019 alipokutwa ofisi kwake akiwa amekufa huku mlango wa ofisi ukiwa umefungwa.
 

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu alikiri kuwapo kwa kifo hicho lakini akasema wasemaji ni Jeshi la Polisi huku akisema katika imani ya dini ya Kiislamu kifo kinaweza kumkuta mwanadamu mahali popote.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo lakini alikuwapo wakati mwili huo unachukuliwa jana Jumatano saa moja jioni ukapelekwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Wananchi wameomba sasa ulinzi uimarishwe na kamera zifungwe majengo yote muhimu jijini Dodoma. Msiba uko nyumbani kwake Mtaa wa Chang’ombe jijini Dodoma.


from MPEKUZI

Comments