Waziri Wa Kilimo Mhe Hasunga Awafunda Wenyeviti Wa CCM Walioshinda Uchaguzi Wa Serikali Za Mitaa Novemba 2019

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Serikali imejipanga kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa na dhamira ya kumkomboa mkulima kwa kuimarisha masoko ya bidhaa zao sambamba na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za uhakika na kwa wakati.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema hayo jana wakati akizungumza na wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi walioshinda kwa kishindo kwa kupita bila kupingwa katika jimbo la Vwawa Mkoani Songwe.

Amesema kuwa moja ya mambo ya msingi katika majukumu yao wenyeviti hao ni kuhakikisha kuwa wanahamasisha wakulima kutumia pembejeo sahihi wakati wa msimu wa kilimo sambamba na kufuata taratibu bora za kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao yao.

Mhe Hasunga alisema endapo wakulima watafuata maelekezo ya wataalamu mbalimbali wa kilimo wataongeza uwezekano mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara jambo litakalopelekea kuimarisha kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga vyema kusimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati huku akiwahakikishia wakulima kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli itawachukulia hatua za kisheria watendaji wote watakaoshindwa kusimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati ili kuendana na msimu wa kilimo.

Alisema kuwa wapo wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wanawauzia wakulima pembejeo feki hivyo amewataka wenyeviti hao kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa haraka iwezekanavyo kuhusu kadhia hizo punde wanapopata taarifa kutoka kwa wananchi.

“Waambieni wakulima wote wawe wanatunza mifuko ya mbegu wanazonunua ili ikionekana hazijaota sisi tushughulike na wote wanaosambaza” Alisisitiza Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Hata shetani alipoasi Mungu alimtupa Duniani pamoja na kwamba alikuwa muimbishaji mkuu wa kwaya ya mbinguni”

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amepiga marufuku wafanyabiashara kwenda vijijini na debe la kupimia mazao badala yake wanapaswa kufuata utaratibu sahihi wa kutumia vipimo vinavyotakiwa ambavyo ni Mizani za Kidigitali.

Aidha, amewataka wenyeviti kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kutojihusisha na rushwa, na ubadhilifu badala yake amewataka kuchochea shughuli za maendeleo, kuwa waadilifu, kujituma na kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji.

Pia Mhe Hasunga amesema kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa umemalizika hivyo amewataka wenyeviti hao kuvunja makundi yote yaliotokana na uchaguzi ili wananchi wote washiriki shughuli za maendeleo na kutekeleza kwa ufasaha ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.


from MPEKUZI

Comments