Walimu 4,046 wa shule za msingi na sekondari wafukuzwa kazi

Katibu Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindurwa amesema jumla ya walimu 4,046 wa shule za msingi na sekondari wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo utoro kazini, kukiuka maadili na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi.

Rutaindurwa ameyasema hayo jana  katika mkutano wa siku mbili uliolenga kuwajengea uwezo Makatibu Wasaidizi wa TSC kutoka Wilaya zote Tanzania Bara uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, jijini Dodoma.

Katika Maelezo ya kumkaribisha Naibu Waziri (Elimu) wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara, Rutaindurwa alisema kuwa tangu TSC ianze kufanya kazi mwezi Julai, 2016 walimu 7,123 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu baada ya kukiuka maadili ya kiutumishi.

“Mheshimiwa Naibu Waziri katika makosa yaliyotendwa kwa kipindi cha miaka mitatu, makosa 5,447 yalikuwa ya utoro kazini, makosa 1,290 kukiuka maadili, makosa 162 uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi na makosa mengine kwa ujumla wake yalikuwa 224”, alieleza Rutaindurwa

Alifafanua kuwa TSC imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kiutumishi kwa mujibu wa Sheria Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu ambapo walimu  4,046 walifukuzwa kazi, walimu 930 walipewa onyo/karipio, walimu 284 walipunguziwa mshahara, walimu 244  walisimamishiwa nyongeza ya mshahara, walimu 237 walishushwa cheo na walimu 14 walipewa adhabu ya kufidia hasara.

Alieleza kuwa walimu wengi walikutwa na makosa ya utoro wakati wa zoezi la uhakiki wa watumishi kwa kuwa waliondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila kufuata taratibu na kuruhusiwa na waajiri wao, hivyo walichukuliwa hatua za kinidhamu.

“Wengi wa walimu waliotiwa hatiani kwa makosa ya utoro, walikuwa wameenda masomoni bila kupata ruhusa kutoka kwa waajiri wao na zoezi la uhakiki wa watumishi lilipofanyia ndipo ikagundulika kuwa ni watoro na mchakato wa kuwachukulia hatua za nidhamu ukaanza,” alisema.

Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Naibu Waziri anayeshughulikia elimu katika ofisi hiyo, Mhe. Mwita Waitara alieleza kuwa TSC bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha walimu wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu za kiutumishi ili wajiepushe na makosa ya kinidhamu.

Aliweka bayana kuwa Serikali haijivunii kuwafukuza kazi walimu wake iliyowaajiri yenyewe ikizingatiwa kuwa bado kuna changamoto ya upungufu wa walimu katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kwa kweli tunasikitika kuwa idadi ya walimu waliofukuzwa kazi ni kubwa, lakini ni lazima watumishi wa umma muelewe kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli haina huruma kabisa na watumishi wazembe wasiozingatia Maadili na Miiko ya kazi yao”, alisema Mhe. Waitara.

Pamoja na hayo, Mhe. Waitara alieleza kuwa walimu wamekuwa na kero na malalamiko mbalimbali yanayosababishwa na kutowajibika kikamilifu kwa baadhi ya watendaji wa wanaoshughulikia masuala yao.

Alieleza baadhi ya kero hizo kuwa ni kucheleweshwa kwa malipo ya kusafirisha mizigo kwa walimu waliostaafu, walimu waliostahili kupandishwa madaraja kutopandishwa kwa wakati, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kukataa kupitisha barua za walimu wanaoomba kuhama kutoka Wilaya moja kwenda nyingine na walimu kutotendewa haki katika mashauri ya nidhamu.

Kutokana na changamoto hizo, Naibu Waziri alipiga marufuku tabia ya baadhi ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ya kuzuia kupitisha barua za walimu wanaoomba uhamisho na kueleza kuwa wao sio wenye mamlaka ya kutoa uamuzi wa ombi la mwalimu anayetaka kuhamia wilaya nyingine.

“Ni marufuku kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzuia kupitisha barua za walimu wanaoomba uhamisho. Wao wanapaswa kupitisha, kuweka maoni yao na kuruhusu maombi hayo yaende kwa mhusika aliyeandikiwa. Mwenye mamlaka ya kukubali au kukataa ombi la uhamisho wa mwalimu ni  Katibu Mkuu, TAMISEMI,” alisisitiza Mhe. Waitara.

Aidha, Mhe. Naibu Waziri aliiagiza TSC kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa orodha ya walimu waliostahili kupandishwa madaraja lakini hawakupandishwa na kuiwasilisha TAMISEMI ili taratibu nyingine ziweze kufanyika.


from MPEKUZI

Comments