Waziri Lugola Ayasimamisha Magari Yaliyotaka Kusababisha Ajali......Dereva Wa Basi Akamatwa, Abiria Warudishiwa Nauli
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameyakamata magari mawili yaliyotaka kusababisha ajali kwa kufukuzana na kulazimisha kuovateki bila ya kuwa na tahadhari katika barabara kuu ya Mwanza Mara.
Magari hayo ni basi lililokuwa na abiri liitwalo Manoni Safaris lenye namba za usajili T800DCU, pamoja na lori namba T865CVJ, yaliyokuwa yanatokea Mwanza kuelekea Mkoani Mara, yalipofika Kijiji cha Nyashishi, Wilayani Busega Mkoani Simiyu yakiwa mwendokasi yakawa yanalazimisha kuovateki bila kuwa na tahadhari.
Waziri huyo akiwa safarini akitokea Wilayani Bunda, leo, alishuhudia magari hayo yakiwa mwendokasi na yakilazimisha kuovateki hali iliyosababisha magari yaliyokuwa yanatokea Mkoani Mara kuyakwepa kwa shida ili kuepusha ajali isitokee.
Baada ya tukio hilo, Waziri huyo alimwelekeza dereva wake kugeuza gari na kuyakimbiza magari hayo hasa basi hilo Manoni Safaris lenye namba za usajili T800DCU, ambalo ndilo lililokuwa na makosa dereva akijua magari yanakuja mbele yake lakini akawa analazimisha kuovateki akilikimbiza lori ambalo lilikua mbele yake.
“Huyu dereva hana tahadhari na mtu hatari sana, alitaka kutuua na pia kuua abiria wa basi hili, lazima afunguliwe mashtaka apelekwe mahakamani na iwe fundisho kwa madereva wazembe wa aina hii, na nimeambiwa na abiria hapa kuwa aliwapuuza baada ya kuambiwa apunguze mwendo,” alisema Lugola.
Waziri huyo alimkamata dereva wa basi hilo na kumtaka atoe leseni yake, kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi Busega kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, na alielekeza abiria wa basi hilo warudishiwe nauli zao na watafutiwe basi lingine ili waendelee na safari.
Dereva wa basi hilo, Marijani Saidi alikiri kufanya kosa na alimuomba msamaha Waziri huyo, hata hivyo alikataliwa kutokana na kuvunja sheria za usalama barabarani na kutaka kusababisha ajali.
Akizungumzia tukio hilo, abiria wa basi hilo, Mwita Machela, alisema walimtaka dereva huyo kuacha kuendesha mwendokasi lakini aliwapuuza na kuendelea na safari.
“Waziri yupo sahihi kutusimamisha maana ametuokoa pia, huyu dereva alikua mwendokasi, tulimuonya aache lakini hakutusikiliza, sasa haraka yake imeishia hapa, na sisi tumepotezewa muda wetu kutokana na uzembe wake,” alisema Lugola.
Waziri Lugola alisimamia kondakta wa basi hilo akiwarudishia nauli abiria hao, pamoja na kuhakikisha wanapandishwa katika mabasi yaliyokua yanapita katika barabara hiyo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment