Waziri Lugola Awakatalia Waliopewa Uraia Makazi Ya Wakimbizi Kushiriki Uchaguzi Serikali Za Mitaa Nchini

Na Mwandishi Wetu, Katavi
WAZIRI wa Mambo ya ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema wananchi waliopewa uraia katika Makazi ya Wakimbizi ya Katumba, Ulyankulu na Mishamo nchini hawatashiriki kugombea na kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwa kuwa maombi yao bado yanafanyiwa kazi.

Akijibu maombi ya raia hao waliopo Kata ya Katumba, Mkoani Katavi, Waziri Lugola alisema maombi yao wanayo na Serikali inayafanyia kazi kwa ukaribu zaidi, hivyo wanapaswa kuwa wavumilivu kusubiri majibu yao.

“Serikali inawajali, inawathamini, na pia maombi yenu tunayo, na tunayafanyia kazi kwa ukaribu zaidi kwa kuwa Serikali ya Rais Dkt. Magufuli ni sikivu, naomba muendelee kusubiri bila kuwa na uharaka wowote,” alisema Lugola.

Akisoma hotuba ya wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ndui Station, Diwani wa Kata hiyo, Seneta Baraka alisema wananchi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutopata haki ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2019.

“Ombi letu kwako mheshimiwa Waziri ni kuturuhusu kufanya uchaguzi katika mazingira haya sawa na ilivyofanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ikiwa haiwezekani basi ombi letu na  changamoto zitatuliwe na tupewe fursa ya kufanya uchaguzi mara baada ya changamoto hizo kutatuliwa,” alisema Baraka.

Baraka alisema raia hao walimuomba Waziri huyo, kubalidilisha hadhi ya eneo la Katumba, Mishamo Mkoani Katavi, na Ulyankulu Mkoani Tabora, kuwa na hadhi ya Serikali ya Mitaa kwa kuwa hadhi ya makazi ya wakimbizi inawanyima fursa nyingi za kimaendeleo.

Maombi mengine waliyoyatoa kwa Waziri huyo ni kukamilisha mchakato wa uraia kwa vijana wao uliofanyika mwaka 2017, wakidai kuwa Serikali ilikamilisha mchakato wa uraia wa awamu ya kwanza uliofanyika mwaka 2007, wapo ambao maombi yao hayajakamilika hadi sasa.

Pia waliomba usajili wa laini za simu kwa wenzao ambao hawajakamilisha mchakato wa uraia ili waweze kupata vitambulisho vya taifa.

Akijibu changamoto hizo, Waziri Lugola aliwaambia raia hao maombi hayo yapo mezani kwake na Serikali inayafanyia kazi kwa ukaribu na watapewa majibu mara watakapomaliza kuyafanyia kazi.

Kwa ombi la usajili wa laini za simu, Lugola alisema hiyo ni haki yao kupata vitambulisho, nakuwaahidi kuwa suala hilo litashughuliwa kwa kuwa zoezi hilo ni endelevu.

Kwa upande wake, Mkazi wa Kata hiyo ambaye alikimbia vita mwaka 1972 akitokea nchini Burundi, Zephania Mshinga ambaye ana umri wa miaka 84, alisema Tanzania ni nchi salama, na pia hayupo tayari kuiacha nchi hiyo ambayo ina amani, utulivu, na watu wakarimu.

“Msiombee vita jamani, nilifika hapa Tanzania mwaka 1972 wakati Burundi kulipokuwa na vita, nashukuru nimepewa uraia na kama nikinyang’anywa uraia huu sina mahali pa kwenda, siwezi kurudi nilipotoka maana miaka mingi imepita, sasa ni mkazi wa hapa, naishukuru Serikali ya Tanzania,” alisema Mshinga.

Waziri Lugola yupo Mkoani Katavi kwa ziara ya siku tano ya kikazi, akikagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na askari na watumishi wa Wizara yake, pamoja na kusikiliza kero za wananchi katika mikutano ya hadhara mkoani humo.


from MPEKUZI

Comments