Serikali Yatoa Onyo Kali Kwa Watendaji Kata

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya Watendaji Kata na askari nchini ambao wamekuwa wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu waliowapa ujauzito wanafunzi na amesema watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ameyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilula Sokoni, kata ya Nyalumbu wilayani Kilolo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

“Wanafunzi bado wanaendelea kupewa ujauzito na kukatishwa masomo yao huku watu waliohusika na vitendo hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu baadhi ya watendaji na askari wamezikalia kesi zao na kushindwa kuwafikisha polisi.”

“Watoto wa kike lazima walindwe ili wamalize masomo yao waje kulitumikia Taifa lao. Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi.”

Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na adhabu iliyowekwa na Serikali ni kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayemuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi hususan waishio vijijini wasikubali kurubuniwa na kugawa ardhi yao kwa watu mbalimbali wanaofika kwenye maeneo yao na kutaka wauziwe ardhi bila ya kuzihusisha mamlaka husika.

“Eneo lenu hili la Ilula ni zuri hivyo msikubali kurubuniwa kuuza ardhi yenu kwa sababau inathamani kubwa. Viongozi wa Kata na Vijiji hakikisheni mnaratibu vizuri na muandae mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro.”

Waziri Mkuu alisema wananchi hao wanatakiwa wawe makini na ardhi na mamlaka zinazohusika na ardhi lazima zihusishwe katika ugawaji wa ardhi kwa sababu wakigawa hovyo watasababisha vijana wao hapo baadaye wakose maeneo ya kilimo.

Akizungumzia kuhusu uboreshwaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu ameahidi ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Ilula ili kuwapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma hizo.

Alisema kituo kitakachojengwa kitakuwa na chumba cha kujifungulia, chumba cha maabara kwa ajili ya vipimo mbalimbali, huduma za mama na mtoto, mapasuaji, wodi ya wanaume na wanawake, aliwataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Waziri Mkuu alisema suala la kuboresha na kusogeza huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi zikiwemo za afya limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye anataka kuona wananchi wakiwa na afya nzuri ili waweze kushiriki ipasavyo katika shughuli zao za kimaendeleo.

Kabla ya kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa mradi wa maji Ilula na kuweka jiwe la msingi. Pia, Waziri Mkuu alikagua shughuli za ukarabati wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi  Ilula.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege aliwahimiza wananchi hao wajiunge katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu ya bure wao na familia zao.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi alisema kuwa awali eneo la Ilula lilikuwa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo yam ogogoro ya ardhi ambayo kwa kushirikiana na watendaji wenzake walifanikiwa kuitatua.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments