Naibu wa Waziri wa Afya Dkt.Ndungulile: JAMAFEST Iwe Kichocheo Ulaji Vyakula vya Asili, Kulinda Afya

Na. Paschal Dotto – Maelezo, Dar es Salaam.
Naibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndungulie ametembelea Maonesho ya Tamasha kubwa la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) na kusisitiza wananchi kutumia zaidi vyakula vya asili ili kupunguza uwezekano wa kupata magionjwa yasisyo ya kuambukiza. 


Dkt. Ndungulie amesisitiza utumiaji wa vyakula vya asili baada ya kutembelea Tamasha hilo jana Septemba 25, 2019 ambapo pamoja na mambo mengine alijionea vitu mbalimbali vikiwemo vyakula vya asili na kuwataka Watanzania kujifunza jinsi ya kutumia kuandaa na kutumia vyakula hivyo ambavyo havina madhara katika mwili. 


“Katika Tamasha hili Watanzania wanapaswa kujifunza njia za asili katika kuandaa chakula ambacho kinaweza kuwasaidia kulinda afya zao”, alieleza Naibu Waziri na kutoa mfano wa kuwepo kwa usindikaji wa chakula na mafuta ya asili yanayotokana na matunda. 


Amesema kuwa masuala ya michezo, sanaa na utamaduni yana uhusiano mkubwa na afya na kuwashauri wasanii kutumia Sanaa kuongelea masuala ya kuimarisha afya kkwa kuwasisitiza wananchi kula chakula bora na kufanya mazoezi ili kufikisha ujumbe kwa Jamii kuhusiana na ulaji bora wa chakula. 


Kwa mujibu wa Dkt. Ndungulile, asilimia 30 ya watoto chini ya miaka mitano wana utapiamlo na wamedumaa huku asilimia 10 ya watu wazima wakiwa na lishe iliyopitiliza (vitambi) na asilimia 30 wanapatwa na magonjwa yasiyo ambukizwa ambayo mengi yanatokana na vyakula visivyo bora. 

Kwa upande mwingine Naibu Waziri Ndungulile ameipongeza Wizara ya Habari, UtamaDUNI, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuandaa Tamasha hilo kwa mafanikio ambapo washiriki kutoka nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeshiriki. Nchi hizo ni wenyeji Tanzania, Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda. 

JAMAFEST ni Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo lilipitishwa katika kikao cha 20 na 23 cha Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilichofanyika mwezi Machi na Septemba 2012.  

Tamasha hili hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili na huzunguka katika nchi wanachama wa EAC. Mpaka sasa Tamasha limekwishafanyika katika nchi za Rwanda (2013) na kuhudhuriwa na washiriki 17,500, Kenya (2015) washiriki 21,000 na Uganda (2017) washiriki 42,600 na sasa linafanyika nchini kuanzia Septemba 21 - 28, 2019.

MWISHO 


from MPEKUZI

Comments