Waziri Lugola Afanya Mazungumzo Na Balozi Wa Canada Nchini.

Na Felix Mwagara, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefanya mazungumzo na Balozi wa Canada nchini, Pamela O’Donnel na kumuakikishia ushirikiano zaidi kati ya Wizara yake na Ubalozi huo nchini.

Mazungumzo hayo ya zaidi ya saa moja yalifanyika ofisini kwa Waziri Lugola, jijini Dar es Salaam, leo ambayo yalijadili masuala mbalimbali ikiwemo uimarishaji wa ushirikiano kati ya Wizara na ofisi ya Balozi huyo nchini.

Waziri Lugola alimuakikishia Balozi huyo kuwa, Tanzania itaendelea kuwa salama kwa kuwa Wizara yake imejipanga vizuri kuendelea kuwalinda raia na mali zao pamoja na wageni wote waishio nchini.

“Mheshimiwa Balozi nashukuru sana kwa kunitembelea, najisikia furaha kwa ujio wako na karibu sana wakati wowote, Wizara yangu pamoja na nchi yangu kwa ujumla tutaendelea kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali,” alisema Lugola.

Kwa upande wake Balozi Sara, alimshukuru Waziri Lugola kwa mazungumzo waliyoyafanya na kumuhakikishia ushirikiano zaidi kati ya Canada na Tanzania.


from MPEKUZI

Comments