Brazil Jumatatu imekataa msaada wa kifedha wa dola milioni 20 wa kusaidia kuzima moto katika msitu wa Amazon kutoka kundi la (G7).
Nchi za kundi la mataifa saba yenye uchumi mkubwa wa viwanda G7 zimeahidi msaada wa dola milioni 20 kupambana na moto huo wakati wakiwa katika mkutano wa kilele mjini Biarritz, Ufaransa.
Lakini Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amemuambia Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ashughulikie nchi yake na makoloni yake.
Macron ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo, aliwasisitizia wenzake kuwa wanapaswa kuupa kipaumbele moto unaowaka katika msitu wa Amazon.
Mbali na fedha hizo, Uingereza kwa upande wake imeahidi kutoa dola milioni 12, na Canada itatoa dola milioni 11 pamoja na ndege za kuzima moto.
Onyx Lorenzoni, mkuu wa shughuli za ofisi ya rais wa Brazil ameiambia tovuti ya habari ya G1 kwamba wanashukuru lakini labda fedha hizo zitafaa zaidi kupanda miti na kuimarisha misitu barani Ulaya, huku rais Bolsonaro akisema hamna msaada unaotolewa bure.
"Macron ameahidi msaada kutoka nchi za kitajiri utumike Amazon. Kwa nini macho yao yote wameyaelekeza Amazon? Wanataka nini huko kwa muda mrefu?," amesema Bolsonaro.
Macron alimjibu Bolsonaro kwa kusema kwamba japo kuwa sehemu kubwa ya Amazon imo ndani ya Brazil, lakini hili ni suala la ulimwengu na ujumbe wake kwa kiongozi huyo ni kwamba ulimwengu hautomruhusu kuangamiza kila kitu.
Waziri wa Mazingira wa Brazil Ricardo Salles awali aliwaambia waandishi habari kwamba wanaukaribisha msaada wa nchi za G7 ili kuukabili moto huo unaoteketeza ekari milioni 2.3 katika msitu wa Amazon. Lakini baada ya mkutano na Bolsonaro pamoja na mawaziri wake, serikali ya Brazil ilibadilisha msimamo wake.
Ingawa asilimia 60 ya msitu wa Amazon imo ndani ya Brazil, msitu huo mkubwa unasambaa pia katika nchi nyingine nane ikiwa ni pamoja na Guiana iliyowahi kuwa koloni la Ufaransa na sasa ni sehemu ya Ufaransa kisiasa na kisheria.
-DW
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment