Waziri Hasunga: Vijana Wakishiriki Ipasavyo Kwenye Kilimo Uchumi Utaimarika

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo anakusudia kuwakutanisha vijana kwa ajili ya kongamano la kujadili fursa zilizopo katika sekta ya Kilimo.

Waziri Hasunga ameyasema hayo tarehe 28 Julai 2019 wakati akizungumza na vijana wa Jimbo la Vwawa katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi makao makuu ya Chama hicho Wilayani Mbozi.

Alisema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanajihusisha na Kilimo lakini miongoni mwao vijana ni wachache hivyo mkakati huo wa kuwakutanisha vijana ni sehemu ya kueleza kwa viajan fursa zilizopo kwenye sekta ya Kilimo na kuziendeleza.

Alisema kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo kuhusishwa kwenye sekta ya Kilimo ni miongoni mwa mambo msingi yatakayoinua uchumi wa vijana nchini kadhalika kuimarisha uchumi wa Taifa.

Mhe Hasunga amesema kuwa vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na mambo yasiyokuwa na tija katika Jamii kama vile kushinda vijiweni badala yake wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha kipato chao kitakachopelekea vijana kutojihusisha na uovu wa aina yoyote.

Kuhusu kuimarisha masoko ya mazao mbalimbali ikiwemo zao la kahawa, Mhe Hasunga amesema kuwa tayari wizara ya kilimo imeanzisha mkakati kabambe wa kuongeza minada ya kahawa ambapo kwa upande wa Kanda ya ziwa mnada utafanyika mkoani Kagera, Kanda ya Kaskazini utafanyika Manispaa ya Moshi, Kanda ya kusini utafanyika wilayani Mbinga na Kanda ya nyanda za juu kusini mnada wa kahawa utafanyika Wilayani Mbozi.

Ameongeza kuwa kuongeza minada ya uuzaji wa zao la kahawa utatoa fursa kwa wakulima kunufaika na mazao yao kwa kuuza kwa bei nzuri na kulipwa kwa wakati.

Mhe Hasunga amewasihi wakulima mkoani Songwe na Taifa kwa ujumla wake kujishughulisha zaidi na Kilimo kwani ndio sehemu pekee yenye uwezo wa kuwaongezea kipato chao.

Kuhusu kadhia ya mbegu feki kwa wakulima Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imejipanga kuimarisha upatikanaji wa viuatilifu kwa wakati na kwa bei nafuu ili wakulima waweze kuvimudu.

"Kumekuwa na mbegu nyingi mtaani ambazo sio sahihi kwa maana hiyo sasa serikali inachukua hatua kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo punde watakapobainika" Alikaririwa Mhe Hasunga

MWISHO.


from MPEKUZI

Comments