Tanzania kuiuzia mahindi Tani Milioni Moja nchi ya Kenya

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema, Serikali itaiuzia nchi ya Kenya mahindi tani milioni moja katika kipindi cha mwaka mmoja, baada ya msimu wa mvua kugoma nchini humo hali inayotishia kuwepo kwa upungufu wa chakula.

Bashe ameyabainisha hayo jana Julai 25,  katika kikao kilichokutanisha idara zilizo chini yake na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo wa Kenya Hamad Boga pamoja na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu.

Ambapo wamekubaliana kwa wiki ijayo watakutana na kufanya kikao kitakachozikutanisha idara zote za mapato na  masuala ya viwango na ubora wa bidhaa kutoka nchi ya Kenya na Tanzania pamoja na sekta zote zinazohusika na mauzo ya chakula.

''Tumekubaliana na wenzetu kwamba mahitaji yao kwa sasa ni Tani milioni moja, sasa hivi NFRA na Bodi ya mazao mchanganyiko wametuthibitishia kuwa wana uwezo wa kuhudumia hilo hitaji la tani milioni moja''

Hatua hiyo imekuja baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Kenya, Profesa Fred Segor, kusema mwaka huu wana changamoto ya hali ya hewa, kwa kuwa mvua haikunyesha ipasavyo.
 
Julai 24, 2019, Rais John Magufuli katika mazungumzo yake na Rais Uhuru Kenyatta, alisema alipomtembelea nyumbani kwake Chato, alizungumzia hitaji la kununua mahindi kutoka Tanzania.


from MPEKUZI

Comments