Rais Magufuli afika Nyumbani kwa kina Mbowe kutoa pole ya msiba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa pole kwa familia, kufuatia kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Albert Lameck Mbowe aliyefariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amekwenda nyumbani kwa Marehemu Salasala Jijini Dar es Salaam na kukutana na familia ikiongozwa na Freeman Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Pamoja na kutia saini kitabu cha maombolezo, Rais Magufuli ameungana na familia hiyo katika sala ya pamoja ya kumuombea Marehemu Meja Jen. Mstaafu Albert Lameck Mbowe.

Baada ya sala hiyo, Rais Magufuli ameitaka familia hiyo iendelee kuwa na umoja na kumtanguliza Mwenyezi Mungu.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo amesema pamoja na kustaafu Meja Jen. Mbowe alikuwa mshauri wa karibu wa Jeshi.

Amesema katika utumishi wake wa miaka 36 na siku 27 Jeshini, Meja Jen. Mstaafu Mbowe alitoa mchango mkubwa katika masuala ya fedha.

Meja Jen. Mstaafu Mbowe alizaliwa Januari 1953, alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1973 na alistaafu utumishi Jeshini mwaka 2009.


from MPEKUZI

Comments