Rais Magufuli achangia Milioni 400 za ujenzi kituo cha afya Morogoro

Rais Magufuli ameahidi kutoa Sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Kisaki kilichopo mkoani Morogoro huku akiwataka wakazi eneo hilo kuchapa kazi.

Magufuli ametoa ahadi  hiyo jana  Alhamisi Julai 25, 2019 wakati akizungumza na wananchi eneo la Kisaki lililopo katika halmashauri ya Morogoro vijijini huku akitoa agizo kwa mawaziri wake, Ummy Mwalimu (afya) na Seleman Jafo wa Tamisemi kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo haraka.

Rais Magufuli alifikia uamuzi huo, baada ya wakazi hao kumweleza hawana kituo cha afya katika eneo hilo.

“Kwanini  hakuna kituo cha afya na kuna watu wengi hapa? Nataka kituo cha afya kianze kujengwe mara moja nitamuagiza Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi) ashughulikie.”

“Nawapa siku saba tafuteni eneo, tujenge hospitali ambayo imejengwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk John Magufuli,” alisema Magufuli huku akishangaliwa na umati wa wakazi wa Kisaki waliojitokeza kumsikiliza.


from MPEKUZI

Comments