Na; Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb) amewataka vijana kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa wazalendo na wenye mshikamano katika kujenga Taifa.
Mhe. Mavunde amesema hayo wakati wa hafla fupi ya kuwaaga vijana kutoka Mkoa wa Songwe, Arusha, Tanga, Kaskazini Unguja na Kusini Unguja kabla ya kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni ishara ya kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Nyerere iliyofanyika Mkoani Kilimanjaro katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Alisema kuwa vijana wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuiga kivitendo yale yote yaliyotendwa na waasisi wa taifa hili, Mwl. Julius K. Nyerere na Hayati Mzee Abeid Karume kwa kuendelea kudumisha upendo, amani na mshikamo kwa mustakabali wa Taifa.
“Vijana waliowengi kipindi hiki wameweka pembeni uzalendo wa kulipenda taifa lao hali ambayo inatubidi tujitahmini na kuenzi falsafa walizokuwa nazo waasisi wetu ambao waliweka maslahi ya Taifa mbele wakati wote,” alisema Mavunde
Akitolea mfano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwatumikia wananchi kwa kutekeleza masuala mbalimbali ya kitaifa wakati wote ili nchi isonge mbele kimaendeleo.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza vijana waliopanda mlima huo awamu ya kwanza na awamu hii ya pili kwa kuonesha ushujaa na uzalendo kwa Taifa lao ikiwemo kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza sekta ya utalii.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde alitoa wito kwa vijana kuacha kukaa kwenye vijiwe na kujihusisha kwenye mambo yasio na tija, bali wajishughulishe kwenye miradi mbalimbali itakayo wawezesha kiuchumi na kusaidia kukua kimaendeleo, kwa kuwa waasisi wa taifa walikuwa wachapakazi, waadilifu na wabunifu ambao ni mfano mzuri wa kuigwa.
“Hakuna nchi yoyote dunia ambayo inaweza kuendelea pasipo kuhusisha nguvu kubwa ya vijana katika maendeleo ya taifa,” alieleza Mavunde
Aliongeza kuwa ili kufikia malengo kwenye uchumi wa viwanda ni lazima vijana wazingatie uzalendo, utaifa na bidii katika kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba alisema kuwa kitendo cha vijana hao kushiriki katika kupanda Mlima huo ni jambo muhimu kwa taifa na inaashiria namna gani vijana wameanza kutambua historia ya waasisi wa taifa lao.
Naye, Kiongozi wa Vijana hao waliopanda Mlima Kilimanjaro Bw. Augustine Gusha aliunga mkono maelezo yaliyotolewa na Naibu Waziri na alitumia nafasi hiyo kuwasihi vijana kudumisha amani ya nchi wakati wote.
Katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2019, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana inaratibu shughuli ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa Vijana 100 kwa ajili ya kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Awamu ya kwanza vijana walipanda mlima huo tarehe 26 Machi, 2019 na awamu ya pili 26 Julai, 2019. Awamu ya Tatu itakuwa mwezi Oktoba.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment