Makamu Wa Rais Kufungua Maonesho Ya Nanenane Kitaifa 2019 Mkoani Simiyu

Na Stella Kalinga, Simiyu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2019, yatakayofanyika Kanda ya Ziwa Mashariki katika Viwanja vya Nyakabindi Mjini Bariadi kuanzia tarehe 29/07/2019 hadi 08/08/2019.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari  katika mkutano maalum wa kutoa taarifa kwa Umma uliofanyika  Mjini Bariadi, Julai 24, 2019.

Mtaka amesema Mhe Makamu wa Rais atafungua rasmi maonesho hayo Agosti Mosi, 2019 na waoneshaji mbalimbali zikiwemo Taasisi, Mashirika mbalimbali na wajasiriamali wataanza kuonesha teknolojia, huduma na bidhaa zao Julai 29, 2019 ikiwa ni maandalizi ya ufunguzi rasmi utakaofanywa na Mhe. Makamu wa Rais.

“Shughuli ya ufunguzi itafanywa tarehe 01/08/2019 na Mhe. Makamu wa Rai, haya ni maonesho ambayo yatakaribisha viongozi wa Kitaifa, Agosti 03, 2019 tutakuwa na Mhe. Waziri Mkuu, Agosti 06, 2019 tutakuwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Kilele tunatarajia kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli” alisema.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba amesema ameridhishwa na maandalizi ya Maonesho ya nanenane yanayoendelea mkoani Simiyu na kutoa wito kwa wakulima na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho haya ili kuja kujionea teknolojia mbalimbali zitakazojibu changamoto za wakulima, wafugaji na wavuvi.

Aidha, Mhe. Mgumba ametoa wito kwa waoneshaji kuwa wabunifu katika teknolojia, huduma na bidhaa watakazoonesha ili maonesho haya yawe  chachu ya kuwasaidia wakulima, wavuvi na wafugaji  kuongeza tija katika uzalishaji

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima amesema matarajio ya mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki ni kuwa na maonesho ya tofauti na mwaka jana, lengo likiwa ni kuifanya kanda hiyo kuwa ni mahali pa kudumu pa wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa na maonesho ya kilimo biashara.

Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanafanyika kwa mara ya pili sasa mkoani Simiyu tangu Kanda ya Ziwa ilipogawanywa katika kanda mbili yaani, Kanda ya Ziwa Mashariki(Simiyu, Mara na Shinyanga) na Kanda ya Ziwa Magharibi(Mwanza, Geita na Kagera) ambapo mwaka huu yanaadhimishwa chini ya kauli Mbiu:-“KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KATIKA UKUAJI WA UCHUMI WA NCHI”

MWISHO


from MPEKUZI

Comments