Mwili wakutwa kichakani umekatwa miguu, mkono na Kiuno

Mtu  ambaye hajafahamika mara moja, amekutwa kichakani akiwa amefariki dunia huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.

Tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Nunga, Kata ya Ngogwa wilayani Kahama baada ya wananchi kuukuta mwili huo ukitoa harufu, huku viungo kama mkono, sehemu za siri na miguu vikiwa vimeondolewa na watu wasiojulikana wanaodaiwa kutekeleza mauaji hayo.

Ofisa Mtandaji wa Kata hiyo, Michael Magoyi, amesema  kuwa tukio hilo, kutokana na hali ya mwili, limetokea siku za karibuni chini ya wiki moja na wananchi walipogundua walitoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji hicho.

"Taarifa ya kuokotwa kwa mwili huo nilizipata kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Nuja ambaye alidai kwamba alipelekewa taarifa hizo na mwananchi aliyefahamika kwa jina la Thomas Shaban. Baada ya kupokea taarifa hizo, nilifika eneo la vichaka kisha nikapiga simu polisi ambao walifika haraka na kuokota kiwiliwili hicho.

Magoyi alisema tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wananchi hasa baada ya watu waliofanya uhalifu huo kukata viungo mbalimbali vya mwili wa mtu huyo kisha kutoweka navyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Richard Abwao, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtu huyo ambaye hajafahamika aliuawa na watu wasiojulikana kisha kutelekezwa porini.

Kamanda Abwao alisema baada ya wauaji kutekeleza tukio hilo, mwili huo waliusambaratisha kwa kuukata vipande vipande na kubakiza kichwa, mkono mmoja na kifua, huku viungo vingine kuanzia kiuno na miguu yake na mkono walitoweka navyo kwa lengo wanalofahamu wao.

Kutokana na tukio hilo, Abwao alisema Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linaendesha msako ili kuwabaini watuhumiwa wa mauaji, huku akiwasihi wananchi lilikotokea tukio hilo, kuwa wepesi kutoa taarifa ili kudhibiti matukio ya namna hiyo.


from MPEKUZI

Comments