Naibu Waziri Mhe.kanyasu Aahidi Mageuzi Kwenye Jumuiya Za Hifadhi Za Wanyamapori

Serikali imewahakikishia Wenyeviti wa Muungano wa Jumuiya za  Hifadhi za Wanyamapori nchini (WMAs) kuwa itaendelea kufanya mageuzi pamoja kuwapa ushirikiano kwa  kuendeleza dhana halisi  ya uhifadhi wa wanyamapori  shirikishi katika jamii.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma  na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Constantine Kanyasu wakati akizungumza na wenyeviti hao kwenye mkutano wa siku moja uliolenga kuimarisha ushirikiano kati ya wizara na wadau hao wa uhifadhi nchini.

Amesema Wizara itaendelea kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwa kuwa inatambua mchango mkubwa wanaoutoa katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori nchini.

Aidha,  Mhe.Kanyasu ameziagiza WMAs zinazotegemea kufanya uchaguzi hivi karibuni  ziendelee na utaratibu wa zamani wa kutumia kigezo cha elimu ya kuanzia darasa la 7 na kuendelea.

 Amesema lengo la  kuruhusu kutumika kwa kigezo hicho cha elimu  ya darasa la saba na kuendelea ni kutoa fursa kwa  wagombea wengi wenye uwezo kuweza kujitokeza.

 Amezitaka WMAs hizo  kuchagua viongozi watakaokua na uwezo wa  kutekeleza  mipango mbalimbali kwa ufanisi.

Hata hivyo, amesema kuwa yapo baadhi ya mambo ya msingi ambayo Wizara imeanza kuyaboresha kwenye kanuni za WMAs  likiwemo suala la kiwango cha elimu kwa viongozi wa WMAs nchini ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima inayojitokeza mara kwa mara ndani ya WMAs hizo.

Kwa upande Mwenyekiti wa Muungano huo, Bw. Christopher Mademula amemueleza Mhe.Kanyasu kuwa suala la kigezo cha elimu liangaliwe kwa mapana yake kwa kigezo kuwa ikiwa wagombea wa darasa la saba hawataruhusiwa kugombea nafasi za uongozi kwenye WMAs, kitendo hicho kitachochea ujangili kwa kuwa wao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za kiinteligensia za ujangili kwenye maeneo yao.


from MPEKUZI

Comments