NACTE Yasitisha Udahili Kozi Ya Hudumu Ya Afya Ngazi Ya Jamii Kwa Mwaka Wa Masomo 2019/2020

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(NACTE)limetangaza kusitisha udahili wa wanafunzi wapya wa program ya Huduma ya Afya Ngazi ya Jamii(Community Health) kwa mwaka wa masomo 2019/2020 hadi hapo itakapotangaza tena.

Akizungumza mbele ya wanahabari Jijini Dodoma  janas Mkurugenzi wa uzingativu, ufuatiliaji na Tathmini wa NACTE Jofrey Oleke, amesema maombi ya udahili kwa waombaji wapya wa Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2019/2020, umesitishwa hadi hapo baraza litakapotangaza maamuzi mengine.

Kufutwa kwa udahili huo kumetokana na maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwamba kwa mwaka huu wa masomo hakutakuwa na kozi hizo.

Kuhusu kusitishwa kwa udahili, amesema baraza limepokea maagizo kutoka wizara ya afya ambao ndio wanaosimamia kozi zote za afya, kuwa katika mwaka huu wa masoma hakutakuwa na udahili katika ngazi hiyo afya ya jamii nasi tunatekeleza.

“Baraza linavitaarifu vyuo na umma kwamba udahili wa wanafunzi katika programu ya Huduma ya afya Ngazi ya Jamii umesitishwa hadi hapo itakapotangazwa tena”,amesema.

Pia baraza limetangaza kufunguliwa kwa udahili mpya kwa ngazi za Astashahada na stashahada kwa kozi zote isipokuwa kwa kozi za ualimu na utaendelea mpaka tarehe 2 mwezi wa tisa mwaka huu kwa vyuo vyote vinavyotoa mafunzo katika ngazi hizo.

Amefafanua kuwa kwa waombaji wa programu za Afya katika vyuo vya Serikali watatakiwa ama kuomba moja kwa moja kupitia vyuoni ambapo vyuo vitasawasajili kupitia baraza la chuo au wanaweza kuomba kupitia tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (www.nacte.go.tz) kubonyeza kwenye ‘apply online'(SAVS).

Kuhusu waombaji wa programu za Afya kwenye vyuo visivyo vya Serikali na waombaji wa programu nyingine zote wanatakiwa kuomba moja kwa moja kwenye vyuo husika.

“Hivyo vyuo vitapokea maombi na kufanya uchaguzi wa wanafunzi wenye sifa na kisha wawasilishe NACTE majina ya waliochaguliwa kwa ajili ya uhakiki kabla ya kuyatangaza, vyuo vinaelekezwa kuzingatia utaratibu wa udahili kama ulivyotolewa na baraza katika mwaka wa masomo 2019/2020,”amesema.

Amewataka wahitimu wote wa Elimu ya Sekondari na vyuo wenye sifa za kujiunga na kozi za Astashahada na Stashahada, kufanya maombi kwa umakini ili kuweza kupata nafasi ya kujiunga programu wanazozipenda na ambazo wanatimiza vigezo/sifa za kujiunga nazo kwa mwaka 2019/2020.

Pia baraza limewashauri waombaji na wazazi kuhakikisha kuwa wanaomba kwenye vyuo vinavyokidhi ubora ambavyo vimeorodheshwa kwenye kitabu cha mwongozo wa udahili kwa mwaka wa masomo mwaka 2019/2020 .


from MPEKUZI

Comments