Kesi ya vigogo 11 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) Yapigwa Kalenda

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi inayowakabili vigogo 11 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) baada ya wakili wa utetezi kuomba muda kupitia jalada.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kukiuka sheria wakati wa ununuzi wa mabehewa 25.

Wakili wa utetezi, Tibita Muganga amedai leo Jumanne Mei 28, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo kueleza kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya usikilizwaji na shahidi yupo.

"Kati shauri hili nashiriki kwa mara ya kwanza baada ya wakili, Malamsha aliyekuwepo awali kujitoa nimeshaanza kazi ya kulipitia jalada ninaomba nipewe muda kidogo kwa ajili ya kumalizia kazi hiyo,” amedai wakili Muganga.

Hakimu Shahidi amekubali ombi hilo na kupanga shauri hilo kusikilizwa Mei 29, 2019 na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Vigogo hao ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu; mkuu wa kitengo cha makenika na mhasibu mkuu, Jasper Kisiraga; kaimu meneja wa usafiri, Mathias Massae; kaimu mhandisi wa ufundi na meneja ujenzi, Muungano Kaupunda na mkuu wa ufundi na meneja ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.

Wengine ni mhandisi mkuu wa ufundi, Paschal Mafikiri;  mhandisi mipango,  Kedmo Mapunda;  kaimu mhandisi wa mawasiliano, Felix Kashaingili; mkuu wa usafiri wa reli, Lowland Simtengu; mkuu wa ubunifu na utengenezaji wa nyaraka, Joseph Syaizyagi na kaimu mkuu wa usafirishaji, Charles Ndenge.


from MPEKUZI

Comments