Auawa kwenye sherehe akigombea mwanamke

Mkazi  wa Mtaa wa Tagota Halmashauri ya mji Tarime mkoani Mara, Muniko Kinyunyi (30) amekufa kwa kuchomwa na kisu shingoni baada ya kutokea ugomvi na mwenzake ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.

Wawili hao wanadaiwa kuwa walikuwa wakigombea mwanamke katika sherehe iliyofanyika nyumbani kwa aliyekuwa mgombea ubunge mwaka 2015 Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki.

Kwa mujibu wa diwani wa Kenyamanyori, Ganga Mgendi tukio hilo la kusikitisha lilitokea usiku wa kuamkia jana nyumbani kwa Kembaki Tarime mjini.

Kembaki katika uchaguzi huo wa mwaka 2015 aliwania nafasi hiyo ya ubunge Tarime Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuangushwa na mbunge wa sasa, Esther Matiko (Chadema).

Mgendi alisema tukio hilo lilitokea wakati wa sherehe iliyofanyika nyumbani kwa mwanasiasa huyo aliyetembelewa na dada yake aliyekwenda na kikundi cha watu kuwasalimia mama na ndugu zake.

Alisema katika shamrashamra hizo ndipo kulipoibuka ugomvi kati ya Mniko na mtu ambaye hakufahamika mara moja jina lake wakigombea mwanamke hali iliyosababisha mtu huyo kumchoma Mniko kisu shingoni karibu na kifuani na kisha kutoroka wakati watu wakihangaika kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya Tarime ambapo alifariki kabla ya kupatiwa matibabu kutokana na kutokwa damu nyingi.

Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Henry Mwaibambe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji na kueleza kuwa Jeshi la Polisi linamsaka mtuhumiwa na kuwaomba raia wema kutoa ushirikiano ili kuweza kumkamta mtuhumiwa huyo aliyetoroka.

Credit: Habarileo


from MPEKUZI

Comments