Pigo kwa Kenya baada ya China ‘kukataa’ kuipa mkopo wa kujenga reli (SGR)

China imekataa kwa mara ya pili kutoa mkopo kwa ajili ya kufadhili awamu ya tatu ya ujenzi wa reli ya kisasa nchini Kenya (SGR) kutoka Naivasha hadi Malaba.

Uamuzi huo wa China wa kukataa kuipa Kenya mkopo huo ambao imekuwa ikiomba kwa muda sasa, unaziweka katika sintofahamu awamu mbili za ujenzi wa reli hiyo (Mombasa hadi Nairobi, na Nairobi hadi Naivasha).

Badala ya kupata mkopo wa kujenga SGR, Kenya imeweza kupata mkopo wa TZS bilioni 906.8 kwa ajili ya kukarabati reli ya zamani (meter gauge) ambayo sasa italazimika kuunganishwa na SGR ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo kutoka Mombasa kwenda Uganda.

Kenya ilikuwa inahitaji mkopo wa TZS trilioni 8 kwa ajili ya kukamilisha awamu hiyo ya mwisho ya ujenzi wa reli hiyo, na kuiunganisha na Uganda.

Kufuatia uamuzi wa China, baadhi ya wataalamu wa uchumi wamesema kuwa sasa Kenya imebakiwa na reli ambayo haiendi popote (a railway to nowhere), huku mkopo uliotumika kutengeneza awamu mbili za kwanza ukitakwa kuanza kurejeshwa.

Waziri wa Usafiri wa Kenya, James Macharia  alisema kuwa wameafikiana na China waikarabati kwanza reli ya zamani, ili SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha itakapokamilika mwezi wa 8, mizigo inayotoka Mombasa iweze kufika Malaba kwa wakati.

Hata hivyo imeelezwa kuwa masharti magumu ndiyo yaliyosababisha Kenya kushindwa kupata mkopo huo, ambapo China ilikata kutoa sehemu za fedha hizo kama ruzuku, lakini pia iimetaka kuwepo na maelezo ya namna reli hiyo itakavyozalisha faida kabla ya kufadhi ujenzi huo wa Naivasha.

Reli hiyo ya Kenya tayari imekamilika katika sehemu ya Mombasa hadi Nairobi huku kipande cha Nairobi hadi Naivasha kikitarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

Tangu kuzinduliwa kwa reli ya Mombasa hadi Nairobi Juni 2017, tayari abiria milioni 2.6 wameshatumia usafiri huo huku mizigo yenye tani 3.6 ikiwa imesafirishwa.

Katika mwaka wake wa kwanza wa kutoa huduma, reli hiyo ilipata hasara ya TZS bilioni 227, ambapo waziri mwenye dhamana alisema hasara hiyo ilitarajiwa kutokana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu usafiri huo.


from MPEKUZI

Comments