Zitto Kabwe amtangaza Juma Duni Haji ‘Babu duni’ Kuwa Naibu Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametangaza kumteua Juma Duni Haji maarufu kama Babu Duni kuwa naibu kiongozi wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ACT-Wazalendo, Kijitonyama, Dar es Salaam leo Machi 26, 2019, Zitto amesema kuwa kwenye kikao cha uongozi wa chama, wameridhia Duni kuwa naibu kiongozi wa chama hicho.

"Nimepewa mamlaka na katiba ya chama kumteua, nikawasilisha kwa uongozi na wameridhia na ataanza kesho kutumikia nafasi hiyo", amesema Zitto.

Duni anashika wadhifa huo ikiwa ni siku chache zimepita tangu alipokabidhiwa kadi ya uanachama ya ACT akiwa pamoja na viongozi wengine kutoka CUF akiwamo Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2015, Duni alihamia CHADEMA na kupitishwa kuwa mgombea mwenza wa urais kupitia CHADEMA ikiungwa mkono na vyama washirika vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vya NCCR-Mageuzi, NLD na CUF. Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, Duni alirejea katika chama chake za zamani cha CUF.


from MPEKUZI

Comments