Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Awataka NHIF Kuwalipa Watoa Huduma Ndani ya Siku 30

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kulipa madeni ya hospitali zinazotoa huduma za bima ndani ya mwezi mmoja.

Ummy alitoa agizo hilo jana, jijini Dar es Salaam, baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi, kusema hiyo ni changamoto wanayokutana nayo katika utoaji wa huduma kwenye jengo la huduma binafsi lililozinduliwa hospitalini hapo.

Mtendaji mkuu huyo alieleza changamoto hiyo wakati wa uzinduzi wa jengo la kutoa huduma binafsi za kibingwa kwa wagonjwa wa nje.

Msangi alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo kwenye utoaji wa huduma binafsi ni ongezeko la wagonjwa, hivyo mifuko ya bima ya afya, ukiwamo NHIF usipotoa malipo kwa wakati husababisha shida kwao.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Ummy, wakati akizindua jengo hilo, alisema alishaielekeza NHIF kwamba kama mtu ameshatoa huduma kwa wateja, alipwe ndani ya mwezi mmoja.

“NHIF mpo hapa? Nataka ndani ya mwezi mmoja muwe mmewalipa watoa huduma kwa wanachama wenu. Kama mtu amefanya kazi mjitahidi mumlipe, maana mnajificha kwenye kivuli cha kuhakiki. Mnahakiki kitu gani kisichoisha?” Alihoji.

“Nanawaomba na nyie watoa huduma mpeleke madai yenu kwa wakati ili wayahakiki mapema,” alisema.

Katika mkutano huo, Waziri Ummy alibaini kwamba tatizo hilo haliko kwa watoa huduma bali NHIF kutokana na CCBRT kueleza kuwa madai ya mwezi uliopita yameshapelekwa NHIF.

“Kumbe tatizo liko kwetu NHIF. Nawaelekeza tusiwe kikwazo cha huduma bora kwa sababu mtoa huduma anategemea hizi fedha kulipa mishahara, kununua vifaa, kulipa umeme na maji. Tunataka watu waone raha ya kuwa na NHIF, sitaki mwisho wa siku watoa huduma waseme hatuzipokei bima kwa sababu malipo hawayapati kwa wakati,” alisisitiza.

Waziri Ummy pia aliwataka Watanzania waone umuhimu wa kuwa na bima kwa sababu ndiyo njia rahisi ya kupata huduma bila kikwazo cha fedha.

Alisema alikutana na kijana ambaye analipa fedha taslimu Sh. 50,000 ili kumwona daktari, gharama ambayo haihusishi vipimo na dawa.

“Nimemwambia NHIF kwa watu sita ni Sh. milioni 1.5, ukiigawa ni kama 250,000 kwa hiyo sisi tumeangalia mkiwa watu sita hawawezi kuumwa wote, kwa hiyo tunakamilisha utaratibu tuwe na bima ya afya ya mtu mmoja mmoja ili kila mtu ajipimie kifurushi chake,” alisema.

Alisema ndani ya wiki tatu, serikali itatangaza vifurushi vya mtu mmoja mmoja ambavyo vitawezesha Watanzania kupata huduma bora za afya.


from MPEKUZI

Comments